1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa hali ya hewa mjini Bonn

Oumilkher Hamidou2 Juni 2009

Wajumbe kutoka nchi 180 wanajadili mkataba badala ya Kyoto

https://p.dw.com/p/I2Di
Misitu inaangamiaPicha: picture-alliance / dpa/dpaweb


Mkutano wa kimataifa kusaka njia za kufikia makubaliano mkutano wa kilele utakapoitishwa mjini Copenhagen nchini Danemark umefunguliwa jana mjini Bonn nchini Ujerumani,wakihudhuria wajumbe zaidi ya 4300 kutoka mataifa 180.

Mswaada wa makubaliano ya mwisho uliopendekezwa wakati wa ufunguzi wa mkutano huo,jana mjini Bonn,ulikosolewa hapo awali na mataifa yaliyoendelea pamoja na yale yanayoinukia,kabla ya maridhiano kufikiwa baadae na kukubaliwa kama msingi wa majadiliano ya mkutano huo utakaoendelea hadi June 12 ijayo.

"Tumeshtushwa na jinsi mswaada huo ulivyoandaliwa" amesikitika mkuu wa ujumbe wa Marekani mazungumzoni Jonathan Pershing,alipokua akizungumzia juu ya mswaada huo wa kurasa 53 unaozingatia mapendekezo ya mataifa yote wanachama wa umoja wa mataifa.

"Lazma pawepo wezani " amesema kwa upande wake Ibrahim Mirghani Ibrahim wa kutoka Sudan, anaezungumza kwa niaba ya nchi zinazoinukia,zinazotanaguliwa na China na India.

Mkutano huu wa Bonn unafanyika miezi sita kabla ya mkutano wa mwisho wa kilele wa mjini Copenhagen,december mwaka huu,unaotazamiwa kupitisha makubaliano yatakayokamata nafasi ya itifaki ya Kyoto.

UN Klimasekretär Yvo de Boer
Mkuu wa halmashauri ya Umoja wa mataifa kuhusu hali ya hewa Yvo de BoerPicha: picture-alliance/ dpa

"Mkutano huu unatoa matumaini mema.Kwa mara ya kwanza kabisa kuna waraka ulioandaliwa ili kuweza kujadiliwa na wawakilishi wa serikali" amesema hayo mkuu wa halmashauri ya Umoja wa mataifa inayoshughulikia masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa Yvo de Boer aliyeongeza kusema:

"Tumeandaa mswaada wa makubaliano na majibu ya mwanzo hayajakawia kutolewa.Ni majibu ya maana.Wajumbe wanauchukulia mswaada huu kua ni muongozo wa majadiliano na nnaamini mswaada huu utatusaidia kufikia makubaliano mjini Copenhagen."

Hata hivyo bwana Yve de Boer amekumbusha kwamba bado kuna vizingiti vinavyobidi kukiukwa.Amesema tunanukuu:Malengo yaliyowekwa na nchi tajiri kiviwanda ya kupunguza moshi wa viwandani hayakutekelezwa vya kutosha".Mwisho wa kumnukuu.

Mswaada uliowasilishwa katika mkutano huu wa Bonn unashauri miongoni mwa mengineyo,nchi tajiri zitenge asili mia mbili ya pato la ndani ili kugharimia miradi itakayozisaidia nchi zinazoinukia kukabiliana vyema na maafa yanayotokana na kuzidi hali ya ujoto mfano mafuriko,vimbunga na balaa la ukame.

Marekani inahisi mswaada huo unaelemea zaidi upande wa nchi zinazoinukia ,na kwamba nchi hizo hazijatakiwa zifanye chochote kuepukana na kuzidi hali ya joto duniani.

Nje ya mahala ambako mkutano huu unafanyika,wanaharakati wa shirika linalopigania usafi wa mazingira Greenpeace waliandamana kuwataka wawakilishi mkutanoni watekeleze kivitendo ahadi zao.

Mataifa yanayoinukia yanayataka mataifa tajiri yapunguze kwa angalao asili mia 40 kiwango cha moshi wa viwandani hadi ifikapo mwaka 2020.

Mwandishi: Oumilkheir Hamidou/RTR/AP

Mhariri:M.Abdul-Rahman