1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa hali ya hewa magazetini nchini Ujerumani

Oumilkher Hamidou10 Desemba 2009

Mivutano imechomoza kati ya nchi tajiri za viwanda na zile zinazoinukia

https://p.dw.com/p/KyrN
Msemaji wa kundi la mataifa 135 yanayoinukia,Lumumba Stanislaus Di-Aping wa kutoka SudanPicha: AP

Mkutano wa kimataifa wa hali ya hewa mjini Copenhagen,waziri wa ulinzi zu Guttenberg akabwa na kisa cha kuhujumiwa malori ya mafuta Kundus na kiu cha kampuni la magari la Ujerumani Volks Wagen kutaka kuwa kampuni kubwa kabisa la magari ulimwenguni ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

Tuanzie lakini Copenhagen ambako mwanya umeshaanza kujitokeza kati ya nchi tajiri kiviwanda kwa upande mmoja na zile zinazoinukia pamoja na nchi maskini za dunia kwa upande wa pili.Gazeti la "OLDENBURGISCHE VOLKSZEITUNG " linaandika:

Kuna mtihani uliochomoza:kimsingi pande zote mbili zina haki.Mataifa tajiri kiviwanda ya magharibi yakiongozwa na Umoja wa ulaya yanaonyesha kulenga makubwa zaidi katika juhudi zao kuliko mataifa maskini na yale yanayoinukia.Hata hivyo kundi la mataifa 77 yanayoinukia-G77 yanazituhumu nchi za magharibi kujiendeleza kiviwanda tangu miongo kadhaa iliyopita na kujihakikishia neema bila ya kujali mazingira.Mataifa yanayoinukia yanahoji kila taifa lina haki ya kujinemeesha.Hoja hiyo ni sawa.Lakini mabadiliko ya hali ya hewa ni ukweli pia uliojitokeza.Ikiwa hayatazuwiliwa,basi madhara yatakua makubwa zaidi katika nchi zinazoinukia.Uwezekano huo wanaujua.Wanajaribu hivi sasa kudai waongezewe viwango va fedha kukabiliana na hali hiyo.Na hiyo pia ni haki.Lakini kinacho hitajika pia ni kuhakikisha fedha zinazotolewa na nchi za magharibi zinatumika ipasavyo."

Mada ya pili magazetini inahusu kitanzi kinachozidi kumbana waziri wa ulinzi wa serikali kuu ya Ujerumani kufuatia kisa cha kuripuliwa malori ya mafuta huko Kundus,kaskazini mwa Afghanistan.Gazeti la "GENERAL Anzeiger" la mjini Bonn linaandika:

Bundesverteidigungsminister Karl-Theodor zu Guttenberg
Waziri wa ulinzi wa serikali kuu ya Ujerumani Karl-Theodor zu GuttenbergPicha: AP

Hadhi ya zu Guttenberg imechujuka.Inaweza kutakasika lakini ikiwa waziri wa ulinzi atajitokeza na kauli thabiti katika suala la kulipwa fidia wahanga wa shambulio la Kundus.Kauli kama hiyo itawakinga wanajeshi wa Ujerumani dhidi ya mashambulio ya jamaa za wahanga wa mashambulio hayo walioghadhibika na pia dhidi ya watalaiban watakaotaka kukitumia kisa hicho.Zaidi kuliko yote,kauli ya waziri wa ulinzi itadhihirisha maadili,heshima na ukarimu."

Mada yetu ya mwisho hii leo magazetini inahusu muungano kati ya kampuni la magari la Ujerumani Volkswagen na lile la Japan Suzuki.Gazeti la "BRAUNSCHWEIGER ZEITUNG" linaandika:

Likiingia njiani kushika bendera ya makampuni makubwa kabisa ya magari ulimwenguni,Volkswagen limepiga hatua kubwa mbele kuliko ilivyokua ikifikiriwa.Lakini ukubwa pekee si ufunguo wa ufanisi.Kama ndio hivyo basi kampuni la Marekani la General Motors lisingefikia hapo lilipo hivi sasa.Kimoja lakini ni dhahiri.Hakuna njia ya kurudi nyuma.VW ni kampuni kubwa kupita kiasi kujiachia kujibanza pembeni.Linalazimika kulenga ukuaji wa kiuchumi katika masoko mepya.Nchini India,soko mojawapo muhimu kabisa kwa siku za mbele,hakuna kinachoweza kufanyika bila ya Suzuki.Ndio maana muungano huo ni wa maana kwasababu watu watajifunza pia namna ya kutengeneza magari madogo madogo kwa bei nafuu barani Ulaya.

Mwandishi:Hamidou Oummilkhheir (Inlandspresse)

Mhariri:Abdul-Rahman