1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa G7: Zelensky ashinikiza mpango wa amani Ukraine

22 Mei 2023

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amehimiza kupewa msaada wa kidiplomasia na kijeshi wakati alipowahutubia washirika wa kundi la nchi saba tajiri ulimwenguni - G7 nchini Japan.

https://p.dw.com/p/4ReV2
G7-Gipfel in Hiroshima
Picha: Stefan Rousseau/AP/dpa/picture alliance

Zelensky alihudhuria mkutano wa G7 mjini Hiroshima ambapo aliutumia muda mwingi akikutana na viongozi wengine wa ulimwengu. Rais wa Marekani Joe Biden pia alikutana na Zelensky na kutangaza msaada wa ziada wa kijeshi wa dola milioni 375 kwa Kyiv.

Baadae jana, Zelensky aliweka shada la maua katika Bustani ya Kumbukumbu ya Hiroshima. Eneo hilo linawakumbuka wahanga wa bomu la atomiki lililodondoshwa na jeshi la Marekani mwaka wa 1945. Ziara ya Kiongozi huyo wa Ukraine katika bustani hiyo ni ya kiishara, wakati kukiwa na hofu kuwa mapigano nchini Ukraine yanaweza kugeuka kuwa mzozo kati ya madola yenye zana za nyuklia.

Soma pia: G7: Ukraine yatawala siku ya mwisho ya mkutano wa kilele

Zelensky aidha alisema kuwa Bakhmut haijakamatwa na Moscow, wakati kiongozi wa mamluki wa Wagner akisisitiza kuwa wapiganaji wake wamechukua udhibiti wa mji huo wote wa mashariki mwa Ukraine.