1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa G7 kutawaliwa na suala la Ukraine

4 Juni 2014

Rais wa Marekani Barack Obama amewasili mjini Brussels Leo(04.06.2014) kwa ajili ya mkutano wa kundi la mataifa saba yenye viwanda duniani , mkutano ambao utagubikwa na suala la mzozo wa Ukraine.

https://p.dw.com/p/1CC95
Obama Rede in Warschau 04.06.2014
Rais Obama akihutubia nchini PolandPicha: Reuters

Obama atakutana na mfalme wa Ubelgiji , mfalme Philip na waziri mkuu Elio Di Rupo kabla ya mazungumzo yake katika chakula cha usiku na viongozi wenzake wa kundi la G7, ambao wameitenga nchi ambayo ilikuwa iwe mwenyeji wa mkutano huo Urusi baada ya nchi hiyo kuliingiza katika himaya yake jimbo la Crimea nchini Ukraine.

Rais Barack Obama leo ameshutumu kile alichokiita mbinu za kizamani za Urusi na ukandamizaji nchini Ukraine na rais Vladimir Putin amejibu kwa kusema , Marekani inatumia mabavu, wakati mashambuliano mapya yakijitokeza katika mvutano mbaya kabisa kuwahi kutokea kati ya Marekani na Urusi kwa muda wa miongo kadha.

Obama Rede in Warschau 04.06.2014
Barack ObamaPicha: Reuters

Akutana na rais mteule wa Ukraine

Obama alikutana leo(04.06.2014) na rais mteule wa Ukraine Petro Poroshenko mjini Warsaw na kuahidi kuiunga mkono kwa muda mrefu nchi hiyo, na kisha akaishutumu Urusi na kuahidi kuyalinda majimbo ya zamani ya iliyokuwa muungano wa kisovieti katika hotuba iliyokuwa na hamasa za kimapambano zaidi ya jumuiya ya NATO kuadhimisha miaka 25 ya demokrasia nchini Poland.

"Miaka25 iliyopita tulishuhudia jambo , ambalo lilikuwa linaonekana haliwezekani. Uchaguzi . Kwa mara ya kwanza watu wa taifa hili walikuwa na fursa. Utawala wa kikomunist ulidhani kuwa uchaguzi utahalalisha utawala wao ama kuudhoofisha upinzani. Badala yake wapiga kura walijitokeza kwa mamilioni . Na kura zilipohesabiwa ulikuwa ushindi wa kishindo kwa uhuru."

Obama und Komorowski Warschau 04.06.2014
Barack Obama(kulia) na rais Komorowski wa Poland(shoto)Picha: Reuters

"Vipi tunaweza kuruhusu mbinu za wakati wa giza za karne ya 20 kuielezea karne hii mpya."

Obama aliuliza , wakati akichukua nafasi ya kuonesha kuwa ni kiongozi wa mataifa ya magharibi , nafasi iliyotumika na marais wa zamani wa nchi hiyo wakati wa vita baridi duniani.

Urusi ilikuwa iwe mwenyeji wa mkutano wa kilele wa kundi la mataifa ya G8 katika mji wa kitalii wa sochi ulioko katika bahari nyeusi , lakini wanachama wengine wa kundi hilo waliamua kufanya mkutano huo kwa kuyashirikisha mataifa saba tu bila ya kuihusisha Urusi mjini Brussels baada ya nchi hiyo kulichukua jimbo la Crimea.

Obama in Warschau 04.06.2014
Obama akiwa mjini WarsawPicha: Reuters

Mkutano kulenga zaidi mzozo wa Ukraine

Rais wa baraza la Umoja wa Ulaya Herman Van Rompuy amesema kabla ya ufunguzi wa mkutano huo wa G7 kuwa mkutano utalenga katika mzozo wa Ukraine na kuitaka Urusi kushirikiana na serikali mpya ya Poroshenko nchini Ukraine.

Obama atakutana uso kwa uso na Putin siku ya Ijumaa nchini Ufaransa. Licha ya kuwa viongozi kadha wa Ulaya watafanya mikutano na kiongozi huyo wa Urusi na kuweka hai matumaini ya kufuata njia ya majadiliano zaidi ili kupunguza mzozo huo wa Ukraine, ambao umeshuhudia mamia ya waasi wakipambana na majeshi ya serikali leo jumatano. Marekani bado haijakubaliana.

Herman Van Rompuy
Rais wa baraza la Ulaya Herman Van RompuyPicha: DW/B. Riegert

"Hatutakubali ukaliaji wa Urusi wa jimbo la Crimea ama ukiukaji wake wa mipaka ya Ukraine, amesema Obama. Obama ameongeza kuwa mataifa huru yataendelea kuwa pamoja ili uchokozi zaidi wa Urusi utakuwa na maana ya kutengwa zaidi na kuigharimu nchi hiyo.

Hatua zaidi kuchukuliwa dhidi ya Urusi

Viongozi hao wa G7 walikuwa wanajitayarisha kujadili hatua yao inayofuata kuhusiana na mzozo wa Ukraine, wakati wanadiplomasia wakitarajia mchanganyiko wa diplomasia na mbinyo.

Ukraine imeshuhudia ikitumbukia katika ghasia tangu mwezi Februari , wakati rais Viktor Yanukovych alipoikimbia nchi hiyo kufuatia maandaano makubwa ya umma kuhusiana na kukataa kwake kutafuta mahusiano ya karibu na mataifa ya Umoja wa Ulaya.

Jumuiya ya kimataifa imeishutumu Urusi kwa kuchochea ghasia za wanaotaka kujitenga katika jimbo hilo la zamani la iliyokuwa umoja wa Kisovieti, ikiwa ni pamoja na kuliunganisha jimbo la Crimea.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / afpe

Mhariri: Mohammed Abdul Rahman