Mkutano wa G7 unaanza mjini Cornwall
11 Juni 2021Sehemu ya viongozi wa wakuu wa mataifa ya kundi hilo wanaendelea kuwasili kwenye hoteli ya fahari ya Carbis Bay iliyo kwenye fukwe za mji wa Cornwall kwa mkutano huo wa G7 utakaojaribu kutafuta majibu kuhusu janga la virusi vya corona na hatua nzito nzito za kuufufua tena uchumi wa dunia.
Rais wa Marekani Joe Biden na mwenyeji wake waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson walikuwepo mjini humo tangu Jumatano na jana walikuwa na mazungumzo mapana kuhusu ushirikiano kati ya Washington na London.
Viongozi wa mataifa mengine ya kundi hilo linalojumuisha pia Ujerumani, Japan, Canada, Italia na Ufaransa walitarajiwa kuwasili Cornwall wakati wowote asubuhi ya leo kwa mkutano huo ambao ni kwanza kufanyika ana kwa ana tangu kuzuka janga la corona karibu miaka miwili iliyopita.
Suala la chanjo za Covid-19 ni kitovu cha majadiliano
Mkutano wenyewe utafunguliwa kwa picha ya pamoja na kufuatiwa na mazungumzo mazito chini ya kaulimbiu ya "Kujiimarisha tena baada ya kizungumkuti cha janga la corona"
Baadae jioni kutakuwa na dhifa ya chakula cha pamoja iliyoandaliwa na Malkia Elizabeth wa Pili.
Duru zinasema viongozi wa G7 watajadili kwa kirefu suala la chanjo za CoVID-19 wakilenga kutoa ahadi ya msaada wa dozi Bilioni 1 za chanjo kwa mataifa masikini na msaada wa kifedha wa kujenga vituo zaidi vya kuzalisha chanjo ulimwenguni.
Viongozi wa kundi hilo wanaandamwa na shinikizo la kuwataka kutangaza mipango ya kutoa msaada wa chanjo kufuatia malalamiko kwamba hakuna usawa katika usambazaji wa chanjo duniani
Kuelekea mkutano huo, rais Biden amesema Marekani itachangia dozi milioni 500 nyingine kwa mataifa 92 masikini na kwa Umoja wa Afrika kabla ya Juni mwaka unaokuja.
"Tutaendelea kuzalisha chanjo, kutoa msaada wa dozi, kutoa ajira, kama wanavyosema hapa Uingereza, silaha mkononi, hadi ulimwengu uvishinde virusi hivi" amesema Biden.
Uingereza nayo itachangia chanjo za Covid-19
Uingereza kwa upande wake imeahidi dozi milioni 100 zitakazotolewa kwa mpango wa usambazaji chanjo kwa usawa wa COVAX unaoratibiwa na Umoja wa Mataifa.
Wakati wa mkutano huo viongozi wa G7 wanatarajiwa pia kujadiliana mikakati ya ulimwengu kujitayarisha vizuri kwa majanga mfano wa Covid-19 kwa miaka inayokuja.
Mbali ya Corona kutakuwa pia na majadiliano kuhusu mabadiliko ya tabianchi na mahusiano kati ya kundi hilo na mataifa ya Urusi na China.
Rais Joe Biden wa Marekani ambaye anahudhuria mkutano wa G7 kwa mara ya kwanza tangu alipoingia madarakani mwezi Januari anatumai kutumia jukwaa hilo kurekebisha dosari za mahusiano na mataifa washirika baada ya miaka minne ya utawala wa misukosuko chini Donald Trump.