Mkutano wa G20 wazungumzia ukwepaji wa kodi
17 Machi 2017Kwa wale washabiki wa kamari za mikahawa ya Casino mjini humo itabidi wasubiri kwa sababu maeneo ya starehe hiyo yatakuwa yamefungwa mpaka Jumamosi jioni.
Sababu ya kufungwa sehemu hizo ni kuwepo kwa mkusanyiko wa viongozi mbalimbali kama vile mawaziri wa fedha,wakuu wa benki kuu wa nchi ishiri zenye nguvu ya kiuchumi duniani.
Ujerumani kwa sasa inashikilia Urais wa kundi hilo la G20, linalowashirikisha nchi 20 muhimu zinazokuwa kiuchumi. Mkutano huo mjini Baden-Baden ni hatua pia , ya kujianda kwa ajili ya mkutano wa kilele wa viongozi unaotarajiwa kufanyika mapema Julai mjini Hamburg.
Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble anatarajiwa kupambana na maswala ya ukwepaji wa kulipa kodi wa makampuni ya kimataifa. Pia sauti yake itasikika katika masuala ya utulivu wa kifedha kupunguza madeni na kutengeneza ushirikiano mpya na Afrika. Kukabilianan na yote hayo, kunahitaji ushirikiano wa kimataifa na ufahamu mzuri juu ya sababu na athari ya vitendo ya kila nchi juu ya nyengine. Lakini kwa upande wa Marekani na sera ya Rais Donald Trump ya " Marekani Kwanza " suala la ushirikiano wa kimataifa kwa sasa linaonekana kuwa gumu.
Kwa umbande wa Africa kundi hilo la G20 limeelekeza katika mchakato wa kuhakikisha kuwa mpango wa kutengeneza sera za kimataifa unakwenda bila ya matatizo.
Mradi wa waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble unaoitwa "Compact with Africa" unaolenga katika uwekezaji, kwa lengo la kutengeneza mazingira bora kwa uwekezaji binafsi katika nchi za Afrika.
Macho yote Washington
Lakini macho yote yako Washington, mbapo kun masuala ya mabishano kama vile ya kupambana na shughuli za benki kinyume cha sheria, ukwepaji wa kodi wa kimataifa, fedha haramu na ufadhili wa ugaidi. Masuala ambayo yatakuwa katika meza ya majadiliano siku ya Jumamosi.
Washiriki katika mkutano wa G20 mjini Baden-Baden ulioanza leo watalenga mtazamo wao mjini Washington, ambako huko Kansela wa Ujarumani Angela Merkel anajianda na mazungumzo yake na rais wa Marekani Donald Trump, katika ikulu ya White House. Bila ya shaka mkutano huo wa viongozi hao wawili huko unaweza kuwa na ushawishi katika majadiliano kwa mkutano wa G20 mjini Baden-Baden.
Mwandishi : Najma Said
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman