Mkutano wa G20 kufungwa kwa wito wa ushirikiano
5 Septemba 2016Washiriki wanatafuta ushirikiano zaidi na maendeleo katika masuala yakiwemo usimamizi wa fedha, biashara ya kimataifa na uwekezaji na pia wanatarajiwa kujadili njia za kupambana na ugaidi na mzozo wa wakimbizi ambapo wanatazamiwa kukubaliana kwamba suala la wakimbizi ni suala la dunia na kwamba mzigo huo unapaswa washirikiane kuubeba.
Kwa mujibu wa rasimu ya mwisho ya makubaliano ya viongozi hao ambayo shirika la habari la Ujerumani dpa imeiona nchi wanachama wa G20 zitajitolea kuhakikisha kwamba ukuaji wa uchumi unakidhi haja ya kila mtu na kuzinufaisha nchi zote na watu wote hususan wanawake, vijana na makundi yaliyokosa fursa, kuzalisha ajira zaidi za maana, kushughulikia suala la ukosefu wa usawa na kutokomeza umaskini ili kwamba kusikuwepo mtu anayeachwa nyuma.
Akifunguwa mkutano huo hapo jana Rais Xi Jinping wa China ametowa wito wa kufanyika kwa juhudi za pamoja kuendeleza ukuaji wa uchumi duniani na kulinda utulivu wa kifedha.
Rais Xi amesema "Tunapaswa kujenga uchumi wa dunia ulio wazi na kuendeleza uregezaji wa masharti ya kibiashara na uwekezaji. Nchi wanachama wa G20 zinapaswa kutimiza ahadi ya kutochukuwa hatua zozote mpya za kuhami masoko na ziimarishe utaratibu na ushirikiano kuhusiana na sera za uwekezaji ili kwamba kuendelea ukuaji wa uchumi kwa vitendo."
Rais Xi pia amewataka washiriki wa mkutano huo kushirikiana ili kupunguza ukosefu wa usawa na ukosefu wa urari katika maendeleo duniani.
Umuhimu wa digitali
Miongoni mwa viongozi wanaohudhuria mkutano huo wa kilele wa G20 ni pamoja na Rais Barack Obama wa Marekani, Rais Vladimir Putin wa Urusi, Waziri Mkuu wa Uingereza Teresa May, Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ambaye amesema viongozi wa nchi za G20 wanaokutana huko China wamekubaliana kwamba inabidi washirikiane kuongeza ukuaji wa uchumi duniani.
Ameyakaribisha mageuzi ya kimuundo ya China wakati nchi hiyo ikishikilia urais wa kupokezana wa kundi hilo la G20 na kusema mawaziri wa masuala ya digitali kutoka nchi hizo zenye maendeleo makubwa ya kiuchumi duniani watakutana kwa mara ya kwanza mwakani wakati Ujerumani itakapochukuwa uongozi wa kundi hilo.
Merkel amesema "Tumetangaza kwamba kuingia kwenye utaratibu wa digitali ni suala muhimu na hatua muhimu ni kichocheo cha ukuaji wa uchumi ambapo mwakani nchini Ujerumani kutakuwepo na mkutano wa mawaziri wa digitali kwa upande wetu na waziri wa uchumi na kwamba kutakuwa na kikosi kazi cha G20 kwa ajili ya ubunifu."
Pamoja na kwamba ukuaji wa uchumi duniani unapiga hatua hatari kutokana na nguvu za masoko, kuzorota kwa biashara, uzalishaji dhaifu wa ajira na masuala mengine yasio ya kiuchumi kama vile ugaidi, mzozo wa wakimbizi na mizizo yanaweka changamoto kwa jamii ya dunia.
Mwandishi: Mohamed Dahman/dpa/AP
Mhariri: Josephat Charo