Mkutano wa G20 kuanza kesho
12 Novemba 2010Rais Barack Obama ameamua kugeuza mtazamo wa mkutano wa G20 na kuuelekeza katika kuangalia hali ambayo haina uwiano sawa duniani na kuziondoa sera za nchi yake katika hali ya kuweza kuchunguzwa zaidi, wakati huu ambapo viongozi mbali mbali duniani wakiwasili mjini Seoul kwa ajili ya mkutano wa mataifa tajiri na yale yanayoinukia kiuchumi ya G20.
Taarifa ya mwanzo ya rasimu ya kundi la mataifa ya G20 iliyodondolewa katika taarifa za soko la hisa la Dow Jones, inakubaliana na pendekezo la mawaziri wa fedha la hapo kabla la kuwa na viwango vya thamani za fedha ambavyo vinabadilika kutokana na thamani ya soko na haionekani kutoa mapendekezo mapya juu ya vipi kupunguza hali ya mivutano kati ya mataifa tajiri yenye matatizo na mataifa yale yanayoinukia kiuchumi, kama China na Brazil.
Obama akiwa anakabiliwa na shutuma kali kutokana na sera za Marekani za kupatikana rahisi fedha wakati akiwasili kwa ajili ya mkutano huo wa siku mbili wa viongozi wa kundi la G20 , amesema kuwa uchumi imara wa Marekani ni muhimu kwa ufufuaji wa uchumi wa dunia, na kuwataka viongozi wenzake wa G20 kuweka kando tofauti zao na kuwajibika ili kuimarisha ukuaji.
Iwapo mataifa yote yatafanya kile kinachostahili kwa upande wao, yale yanayoinukia, ama yale yaliyoendelea, yenye ziada, ama yale ambayo yana nakisi, sote tutafaidika kutokana na ukuaji mkubwa, amesema Obama katika barua iliyotumwa kwa viongozi wa G20 siku ya Jumanne.
Hatua hiyo ya kuleta maelewano imekuja baada ya malumbano makali ya siku moja wakati wajumbe wa majadiliano walipokuwa wakihangaika kupata taarifa ya pamoja ambayo viongozi wote wa G20 wanaweza kutia saini. Mgawanyiko mkubwa umejitokeza kutokana na sera za kiuchumi, hususan uamuzi wa Benki kuu ya Marekani wiki iliyopita kuingiza zaidi ya dola bilioni 600 katika uchumi wa nchi hiyo. Baadhi ya wataalamu wanaona kuwa hatua hiyo huenda ikaleta mzozo mwingine wa kiuchumi duniani.
Uchapishaji mkubwa wa fedha ama uingizaji wa fedha nyingi katika uchumi, huleta hali bora mwanzoni. Lakini baadaye thamani ya fedha huporomoka. Sioni njia ambayo inaweza kuepusha mfumko wa bei iwapo unachapisha fedha kwa wingi.
Viongozi wa kundi la G20 wana matumaini kuwa mkutano wa wiki hii utakuwa ni mwanzo wa enzi mpya ya ushirikiano wa kimataifa. Korea ya kusini ambayo ni mwenyeji wa mkutano huo imechapisha mabango yenye kauli mbiu isemayo , "Ukuaji sawa wa kiuchumi bila mizozo".
Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Miraji Othman