1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa G20 kuanza kesho.

Sekione Kitojo1 Aprili 2009

rais barack Obama wa Marekani na waziri mkuu Gordon Brown wa Uingereza wameeleza matumaini yao makubwa katika kupatikana makubaliano ya dunia ili kujitoa katika mporomoko wa kiuchumi.

https://p.dw.com/p/HOR7
Rais Barack Obama na mkewe Michelle Obama wakipunga mkono wakati walipowasili mjini London tayari kwa mkutano wa kundi la G20.Picha: AP


Rais Barack Obama wa Marekani na waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown wameeleza matumaini yao makubwa kuhusu kupatikana makubaliano ya dunia ili kujitoa katika mporomoko wa uchumi, wakijaribu kupunguza wasi wasi wa kutokea mgawanyiko na rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy, kuhusiana na mafanikio ya mkutano wa kundi la mataifa ya G20 unaotarajiwa kuanza kesho.


Wakati Obama anasema kuwa ana hakika kuwa mkutano huo utafikia muafaka , Sarkozy ameonya kuwa Ufaransa na Ujerumani hazitakubali ahadi hewa, akishauri kuwa makubaliano sio kitu cha kupatikana juu juu tu.

Marekani inataka mipango ya kichocheo cha uchumi, lakini mataifa mengi ya Ulaya badala yake yanataka kulenga katika kupatikana kanuni kali za udhibiti wa sekta ya kifedha.

Mzozo huo, ambao Obama anadai umekuzwa mno , umepunguza matumaini ya kile kinachoweza kufikiwa katika mkutano huo wa London, ambao unaanza kwa chakula cha usiku baadaye leo.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema leo kuwa anaimani kuwa viongozi wa kundi hilo la mataifa ya G20 katika mkutano wao mjini London watachukua hatua , na kuongeza kuwa hawaweze kumudu kuficha vichwa vyao mchangani.

Hata hivyo , ameonya kuwa viongozi hao wa dunia hawapaswi kukubali muafaka dhaifu , akisema kuwa ana wasi wasi kuwa mataifa muhimu hayajatambua ni kiasi gani hali ya kuporomoka kwa uchumi wa dunia ilivyo.

Nakwenda mjini London nikiwa na mchanganyiko wa uhakika na wasi wasi, Merkel amewaambia waandishi habari mjini Berlin kabla ya kwenda mjini London.

Akiulizwa kuhusiana na tishio la rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy la kutoka mkutanoni iwapo matokeo hayatatosheleza matumaini, Merkel amesema kuwa anaunga mkono nia ya rais Sarkozy ya mkutano huo kutokumalizika kwa kupata makubaliano dhaifu.

Hata hivyo msemaji wake baadaye aliufahamisha mkutano wa kawaida na waandishi habari kuwa kitisho cha kutoka mkutanoni sio wazo zuri.

Hata hivyo amekataa miito kwa Ujerumani kuchukua juhudi zaidi kujiondoa kutoka katika mporomoko wa uchumi , akisema kuwa mipango ambayo tayari imekubaliwa inapaswa kupewa muda kuingia katika mfumo wa jamii.

Lakini Ujerumani imejikuta ikishambuliwa na wanachama wengine wa kundi la G20 ambao wanadai kuwa nchi hiyo ambayo ni muuzaji mkuu wa bidhaa nchi za nje haijafanya vya kutosha kuuondoa uchumi wake katika hali ya kuporomoka.


Mwandishi:Sekione Kitojo

Mhariri:M. Abdul-Rahman.

►◄