Mkutano wa G-20 na wafanyafujo magazetini
11 Julai 2017Tunaanzia Hamburg ulikomalizika jumamosi iliyopita mkutano wa kilele wa viongozi wa mataifa 20 yenye nguvu zaidi kiuchumi duniani-G-20. Mhariri wa gazeti la "Mannheimer Morgen" anauwekea suala la kuuliza mfumo wa demokrasia katika mkutano kama huo wa mataifa 20 katika wakati ambapo kuna mataifa karibu 200 duniani. Gazeti linaendelea kuandika: "Meza ya duwara inatajwa kuwa chombo kimoja wapo muhimu cha demokrasia. Lakini demokrasia hiyo ikoje katika mkutano wa kilele wa mataifa 20 wakati ulimwengu una karibu mataifa 200? Ndo kusema ni meza ya duara ya mataifa yenye nguvu zaidi yanayoinyamazisha asili mia 90 ya jumuia ya kimataifa? Katika mkutano wa G-20 kipa umbele ni wale wanaoshika bendera-na taarifa ya mwisho iliyochujwa imebainisha shida za kufikia maridhiano hata miongoni mwa mataifa 20. Kutokana na sababu hiyo mtu anaweza kusema ni hatua ya busara kuwekewa kikomo idadi ya washiriki mazungumzoni.
Wafanyafujo wasakwe na kuandamwa kisheria
Machafuko yaliyokithiri yameugubika mkutano huo wa kilele wa G-20 katika mji alikozaliwa kansela Merkel Hamburg. Mjadala umezuka kuhusu hatua za usalama katika mikutano kama hiyo ya kilele. Gazeti la "Rhein-Necker-Zeitung" linaandika: "Wafanyafujo walidhamiria tangu mwanzo kufanya maovu na walijiandaa kikamilifu kwaajili hiyo. Halikuwa tukio la sadfa lililosababisha maandamano kama yale. Na tukizingatia upande wa pili pia, maafisa wa usalama wa Hamburg hawakufanya vya kutosha kupunguza fujo. Ndio maana makosa yanabidi yatafutwe pia upande wa polisi. Watu kujikosoa ni jambo la kawaida katika demokrasia. Kwa upande mwengine na wafanyafujo pia wanabidi ikiwezekana wajulikane ni nani na waandamwe kisheria.
Enzi za IS zimekwisha
Mada yetu ya pili magazetini inahusiana na kukombolewa mji wa Mosul, mji wa pili kwa ukubwa nchini Iraq uliokuwa ukidhibitiwa na wanamgambo wa itikadi kali wanaojiita wa "dola la kiislam"-IS.Gazeti la "Rheinpfalz" linaandika: "Kwa kukombolewa mji wa Mosul na kuendelea awamu ya mwisho ya hujuma za kuukomboa mji wa Raqaa nchini Syria, itatoweka pia picha waliyojichorea IS ya utawala wao wa kidini-Khalifa. Cha kuhofia lakini ni kile kitisho cha maelfu ya wanamgambo kujificha na kuibuka kwengineko, mfano nchini Libya-nchi iliyoteketezwa kikamilifu tangu mwaka 2011 baada ya jumuia ya kujihami ya NATO kuingilia kati. Kuna uwezekano wa Al Qauda kufufuka ikiwa riopoti zitaathibitika kwamba kiongozi wa Is, al Baghdad kweli amefariki dunia. Hamza bin Laden, mtoto wa kiume wa muasisi wa al Qaida, Osama bin Laden ameshaanza tangu sasa kuvikwa kilemba cha mkuu wa wanajihadi ulimwenguni.
Mhariri:Hamidou Oummilkheir/Inlanmdspresse
Mhariri:Yusuf Saumu