Mkutano wa COP24 waelekea ukingoni bila ya muafaka
14 Desemba 2018Wajumbe kutoka takriban mataifa 200 wanaohudhuria mkutano huo ambao unafika ukingoni leo jioni baada ya kudumu kwa majuma mawili bado wanatofautiana kuhusu masuala muhimu kuanzia suala la ufadhili wa mikakati ya kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi na namna ya kuzisaidia nchi ambazo tayari zinakabiliwa na athari hizo.
Mawaziri walioko katika mkutano huo wa COP24 wanapaswa kukubaliana kuhusu msimamo wa pamoja juu ya namna ya kutekeleza ahadi zilizotolewa na nchi katika mkutano wa mwaka 2015 uliopelekea kufikia makubaliano kuhusu tabianchi ambapo nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ziliahidi kupunguza ongezeko la joto duniani kwa kudhibiti utoaji wa gesi chafu hasa itokayo viwandani.
Nchi tajiri na masikini zavutana
Huku wanasayansi wakionya kuwa kuna haja ya dharura ya kupunguza joto duniani ili kuweza kufikia malengo ya kudhibiti viwango vya joto visipindukie nyuzi 1.5, wajumbe wa mkutano huo wa COP24 wanahimizwa kuchukua hatua madhubuti na za dharura la sivyo nchi hasa masikini zitaanza kushuhudia athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi.
Nchi zinazoendelea zimesema hazitaweza kumudu uchumi wao kwa kugeukia nishati jadidifu bila ya kupata ufadhili wa wazi na unaoaminika kutoka kwa mataifa tajiri. Katika rasimu ya makubaliano yanayotarajiwa kutangazwa saa chache zijazo, hakujatajwa suala hilo la ufadhili kwa mataifa yanayoendelea.
Kupunguzwa kwa gesi chafu ya Carbon na kuzisaidia nchi kujitayarisha kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa katika siku za usoni ndizo nguzo mbili muhimu za mkutano huo wa Umoja wa Mataifa.
Tayari nchi kadhaa zinakumbwa na ukame, mafuriko, vimbunga, misitu kuchomeka, vina vya maji ya bahari kuongezeka na wanyama na mimea adimu kuangamia.
Ujerumani ina matumaini
Waziri wa mazingira wa Ujerumani Svenja Schulze amesema wameingia mkondo wa mwisho wa mazungzumzo lakini sio kila mmoja amefurahishwa na yanayofikiwa lakini ameongeza kusema ana matumaini watafikia makubaliano ya tija licha ya kuwa sio kila nchi inaridhia.
Marekani, Saudi Arabia na Kuwait zinapinga baadhi ya vipengele vya makubaliano ya Paris. Ufafanuzi zaidi unahitajika kuhusu ni jinsi gani nchi zitaimarisha mikakati yao ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi baada ya mkutano huo wa Poland ili kutimiza malengo yao kuambatana na makubaliano ya Paris ifikapo mwaka 2020.
Wajumbe wa kutoka mataifa ya Afrika wanasema bara hilo sharti liwashirikishe wanawake na wasichana katika kufikia malengo ya kuyaokoa mazingira. Utafiti unaonesha kuwa iwapo wanawake wanashirikishwa katika maamuzi, basi mipango ya kuyaokoa mazingira na miradi ya kulinda mali asili kama maji na misitu hufanikiwa zaidi.
Benki ya maendeleo ya Afrika imesema iwapo Wanawake wa Afrika wanapewa elimu na ufadhili, basi watachangia pakubwa katika kupatikana suluhisho la kiteknolojia na kulipeleka bara hilo katika matumizi ya nishati jadidifu.
Mwandishi: Caro Robi/Reuters/Afp
Mhariri: Mohammed Khelef