1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa COP23 wakamilika Bonn

17 Novemba 2017

Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu utekelezaji wa makubaliano ya Paris ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi unakamilika leo baada ya wiki mbili za mazungumzo

https://p.dw.com/p/2nnEI
Deutschland Weltklimakonferenz COP23
Picha: DW/I. Anastassopoulou

Wajumbe kutoka karibu nchi 200, wakiwemo wajumbe kutoka Marekani, walikusanyika katika mkutano huo wa Bonn ili kujadiliana kuhusu sheria zitakazoidhinishwa mwaka ujao, kwa ajili ya kuanza kutekelezwa mkataba wa kimataifa mwaka wa 2015.

Wajumbe wameelezea mchanganyiko wa hisia kuhusiana na mafanikio ya mkutano huo wa Bonn., huku migawanyiko ikiibuka tena kati ya nchi tajiri na zinazoinukia kiviwanda.

Suala linalozusha utata ni kuhusu ufadhili wa mataifa maskini zaidi duniani kuyasaidia kujiandaa na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi – ikiwa ni pamoja na vimbunga vikubwa vya mara kwa mara, kiangazi, na kupanda kwa viwango vya bahari.

Kizingiti kingine kilikuwa ni msisitizo wan chi zilizostawi – zikiongozwa na Marekani – kuwa nchi zite zina majukumu sawa chini ya makataba wa Paris, wakati mataifa yanayostawi na ambayo yanatoa gesi chafu yanataka aina Fulani ya unafuu.

UN-Klimakonferenz 2017 in Bonn | Angela Merkel, Bundeskanzlerin
Ujerumani ina nia ya kupunguza matumizi makaa ya mawePicha: Getty Images//L. Schulze

Kongamano hili liloanza Novemba 6, ni la kwanza la Umoja wa Mataifa kuhusu tabianchi tangu Rais Donald Trump alipotangaza mwezi Juni kuwa Marekani itajiondoa katika makubaliano yaliyopigiwa debe na mtangulizi wake Barack Obama. Sheria zinasema kuwa itaweza tu kujiondoa mnamo Novemba 2020, na kwa wakati huu, serikali yake inaendelea kukaa kwenye kiti chake katika mazungumzo ya tabianchi.

Mjumbe wa Marekani, Kaimu Naibu waziri wa masuala ya Bahari, Mazingira Kimataifa na Sayansi Judith Garber, amesema kuwa ijapokuwa Rais wa Marekani Donald Trump anapanga kujiondoa katika makubaliano ya Paris, Marekani bado iko mstari wa mbele katika matumizi ya nishati jadidifu na uvumbuzi. Kihistoria, Marekani ndio imekuwa ikiongoza kwa uzalishaji wa gesi chafu duniani, ingawa sasa ni pili baada ya China

Mkataba huo unazitaka nchi zilizosaini zipunguze kiwango cha wastani cha joto duniani hadi chini ya nyuzijoto mbili ili kuepusha athari mbaya kabisa za mabadiliko ya tabianchi.

Mataifa yaliwasilisha ahadi za kupunguza kwa hiari utoaji wa gesi chafu ili kuuongeza nguvu mkataba huo, lakini wanasayansi wanasema ahadi hizo zinauweka ulimwengu kwenye mkkondo wa kuwa na kiwango cha nyuzijoto 3 au Zaidi.

Vipi na lini tathmini ya ahadi za nchi ili kuzileta kwenye mkondo wa nyuzijoto 3, ni mada kuu inayojadiliwa katika mazungumzo haya. Nchi 20 na majimbo mawili ya Marekani yamejiunga na muungano wa kimataifa wa kuondoa matumizi ya makaa ya mawe katika uzalishaji wa nishati kabla ya mwaka wa 2030.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu