Mkutano wa COP 24 waingia hatua muhimu ya mwisho
10 Desemba 2018Wakati huo huo Ufaransa imeelezea wasiwasi wake kwamba nchi fulani zitatumia vibaya maandamano yanayofanyika nchini mwake yanayojulikana kama "vizibao vya njano” ili kuzuia matarajio yake katika kupambana na ongezeko la joto duniani. Waziri wa Ufaransa anayeshughulikia masuala ya ekologia endelevu Brune Poirson, pembezoni mwa mkutano huo wa Umoja wa matifa kuhusu mazingira huko nchini Poland, amesema ni vigumu kuyalaumu mazingira katika mgogoro huo unaohusiana na masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Maandamano hayo yamesababisha kutolewa miito ya kumtaka rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aondolewe madarakani kwa madai yakuwapendelea matajiri.
Kuanzia wiki iliyopita, wajumbe kutoka chini ya mataifa 200 wanashiriki mazungumzo hayo yanayofanyika mjini Katowice, Poland ambayo yanaangazia kuyaongezea nguvu masharti ya kugharamia utekelezaji wa mkataba wa Paris uliofikiwa mwaka 2015.
Mawaziri wanatarajiwa kwenye mazungumzo hayo kujadiliana juu ya kuyatekeleza malengo ya kulinda mazingira. Mkuu wa mkutano huo ambaye ni waziri mdogo wa mazinjgira wa Poland Michal Kurtyka amesema mpaka sasa kuna mengi yamefanyika lakini pia bado kuna mengi yanayostahili kufanyika.
Tangu wiki iliyopita, wajumbe kutoka takriban nchi 200 wamewasili nchini Poland kwa mazungumzo hayo ya hali ya hewa ya COP24. Mkataba wa Paris wa mwaka 2015 unatoa muhtasari kwa nchi zinazoshirikiana katika kupunguza kiwango cha joto la dunia kati ya nyuzi joto 1.5 na 2 Celsius.
Jitihada nyingi za kuzuia sayari kupata joto zaidi zinahusiana na kupunguza kiwango cha gesi za chafu haraka iwezekanavyo.
Makubaliano ya sheria yanatarajiwa kufikiwa siku ya Ijumaa, ingawa huenda mkutano muhuimu wa hali ya hewa unaweza kuchukua muda mrefu kuliko iliyopangwa. Hadi sasa mazungumzo hayo yanasuasua, huku wanaharakati wa mazingira wakisema kuwa hayajapiga hatua.
mwandishi:Zainab Aziz/DPAE/AFPE
Mhariri:Yusuf Saumu