Mkutano wa chama cha Republican kufunguliwa Charlotte
24 Agosti 2020Wajumbe wa chama cha Republican nchini Marekani wanaanza kukutana leo huko Charlotte kwenye jimbo la North Carolina, ambapo wanatarajiwa kumteuwa Rais Donald Trump kama mgombea wao katika uchaguzi mkuu wa urais mwezi Novemba. Kwa kipindi cha siku nne wajumbe hao watajaribu kuwashawishi Wamarekani kuwa rais huyo anastahili kuongoza kwa muhula wa pili.
Mkutano huo wa siku nne ni muhimu kwa rais Donald Trump ambaye yuko nyuma ya Biden kwenye kura nyingi za maoni ya kitaifa. Wasaidizi wake wana matumaini kwamba hafla hiyo itawapa nafasi ya kuyaangazia mafanikio ya muhula wa kwanza wa Trump na kuendesha kampeni kuhusu mtizamo wake wa mustakbali wa Marekani.
Rais Trump ana ''mtizamo ulio bora''
Ronna McDaniel, mwenyekiti wa mkutano huo wa chama cha Republican amesema kwamba mkutano huo ni uzinduzi wa wiki kadhaa za kampeni ya uchaguzi. Na kuendelea kusema hadhani watapunguza kasi.
Kwa upande wake raisTrump anaamini mkutano huo utakuwa wa mafanikio. Akiwasili kwenye hafla hiyo, Shirlene Ostrov, mkuu wa chama cha Republican kutoka jimbo la Hawai amesema wana cha kujivunia kuhusu utawala wa Trump.
''Nafikiri raia wa Marekani wataonyeshwa mtizamo mwingine wa Marekani kutoka kwa rais Trump ukilinganisha na huo wa wanachama wa chama cha Democratic. Mtizamo ulio bora, mkubwa na unaovutia kwa nchi yetu.''
Melania Trump kuhutubia hafla ya WaRepublican
Mwaka huu mkutano wa chama umefanyika katika mazingira ya kipekee kwa vyama vyote viwili kutokana na janga la COVID-19. Mara nyingi huwa inakusanya maelfu ya wajumbe, viongozi wa vyama, wadau, waandishi habari na wapenda siasa. Mkutano wa chama huwa ni wiki ya hotuba, sherehe na uchangishaji fedha kwa ajili ya mgombea. Lakini janga la Covid-19 limebadili kila kitu,licha ya kwamba Trump alijaribu kushikilia msimamo wake kuhusu mkutano wa chama hicho.
Ni takribani wajumbe wa Republican 336 pekee, kati ya zaidi ya 2,500 watakaokuwa Charlotte, Jumatatu. Kila jimbo litawakilishwa na wajumbe 6. Baada ya hapo mkutano wa chama hicho utahamia kwenye maeneo yanayofanya matukio kwa njia ya video.
Hatua kali za kiafya zilichukuliwa ili kuepusha maambukizi ya virusi vya Corona. Wajumbe wametakiwa kuheshimu kanuni hizo na walifanyiwa vipimo kabla ya kusafiri.
Wanafamilia wengine wa Rais Trump watazungumza kwenye matukio mbali mbali wiki hii, akiwemo mkewe Melania Trump ambaye anatarajiwa kuzungumza kesho Jumanne akiwa ikulu ya white house. Makamu wa rais Mike Pence atahutubia wajumbe toka mji wa Fort McHenry jimboni Baltimore.
Rais anatarajiwa kuonekana kila siku usiku kuanzia Jumatatu, na siku ya Alhamisi atatoa hotuba akiwa ikulu mjini Washington kukubali rasmi uteuzi wa chama kuwania muhula wa pili madarakani.