Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kumalizika leo
27 Septemba 2021Mwakilishi wa serikali iliyopita ya Afghanistan kwenye Umoja wa Mataifa, Ghulam Isaczai, anatarajiwa kuupinga utawala wa Taliban kwa kuhutubia siku ya Jumatatu, baada ya kundi hilo kuomba waziri wake mpya wa mambo ya nje aruhusiwe kuhutubia badala yake.
Jumatatu iliyopita, kundi la Taliban lilimuandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa, Antonio Guterres likimuomba Amir Khan Muttaqi aruhusiwe kushiriki.
Barua hiyo ilieleza kuwa Isaczai, mjumbe wa Afghanistan kwenye Umoja wa Mataifa chini ya utawala wa Ashraf Ghani aliyeondolewa mdarakani mwezi uliopita, haiwakilishi tena serikali ya Afghanistan kwenye umoja huo.
Ombi hilo lilikuwa linatarajiwa kufikiriwa na kamati inayozihusisha Marekani, Urusi na China, lakini afisa wa Umoja wa Mataifa amesema mkutano huo haukufanyika. Afisa huyo amesema Taliban walichelewa kutuma ombi lao na hivyo kumsafishia njia ya kuzungumza, Isaczai ambaye bado umoja huo unamtambua kama mwakilishi wa Afghanistan.
Awali wiki ya kutolewa hotuba kwenye Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa ilitarajiwa kuhitimishwa na hotuba za viongozi wa Afghanistan, Myanmar na Guinea, lakini hali imebadilikia baada ya nchi mbili pia kusababisha mtafaruku dakika za mwisho.
Balozi wa Myanmar azuiwa kuzungumza
Mwanadiplomasia wa ngazi ya juu katika Umoja wa Mataifa, amesema makubaliano yamefikiwa kati ya Marekani, Urusi na China kumzuia balozi wa Myanmar kwenye umoja huo Kyaw Moe Tun, anayeunga mkono vuguvugu la demokrasia ambaye alikataa agizo la serikali ya kijeshi lililomtaka asihutubie.
Tun ambaye alichaguliwa na utawala wa kiongozi wa zamani wa Myanmar, Aung San Suu kyi, anaungwa mkono na jumuia ya kimataifa na ameshikilia wadhifa wake katika Umoja wa Mataifa tangu yalipofanyika mapinduzi ya kijeshi februari, Mosi. Mwezi Mei, uongozi wa kijeshi ulimteua jenerali wa zamani kuchukua nafasi yake, lakini Umoja wa Mataifa bado haujaidhinisha uteuzi wake.
Hata hivyo, wanadiplomasia wanatarajiwa kusikia kutoka kwa mwakilishi wa Guinea kwenye Umoja wa Mataifa, Aly Diane, ingawa aliteuliwa na rais wa zamani, Alpha Conde ambaye aliondolewa madarakani katika mapinduzi ya kijeshi mwanzoni mwa mwezi huu.
Katika hali nyingine mkutano huo umeshuhudia takribani viongozi 100 wa dunia wakihudhuria ana kwa ana baada ya mwaka 2020 kufanyika kwa njia ya video kutokana na janga la virusi vya corona.
Hata hivyo, viongozi wengi waliziwasilisha hotuba zao kwa njia ya video. Awali Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron alikuwa ahudhurie, lakini aliamua kutuma ujumbe kwa njia ya video ambao uliwekwa siku moja baada ya Rais wa Marekani, Joe Biden kuzungumza.
Ufaransa na uhusiano wake na Marekani
Lakini siku ya Jumatatu Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian atazungumza kwa niaba ya Ufaransa, ambao uwepo wake wiki nzima uligubikwa na mzozo kati yake na Marekani kuhusu makubaliano ya nchi hiyo kuiuzia Australia nyambizi zinazoendeshwa kwa nishati ya nyuklia. Hata hivyo, hotuba yake itatolewa kwa njia ya video, licha ya kuwepo mjini New York.
Kwa ujumla hadi mwishoni mwa Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa, zaidi ya hotuba 200 zitakuwa zimetolewa, nyingi zikiangazia ushirikiano wa kimataifa katika mabadiliko ya tabia nchi na janga la COVID-19.
(AFP)