Takriban wajumbe 1,600, wanaowakilisha wanasiasa na viongozi wa
kidini nchini Afghanistan wanahudhuria mkutano wa amani
unaojulikana kama ''Jirga'' ulioanza siku ya Jumatano mjini Kabul,
ambao wanasema kuwa mazungumzo na Wataliban ndio uamuzi
mzuri na inawezekana kuwa nafasi ya mwisho ya kupatikana amani
nchini humo.
Kiongozi wa baraza la Ulemaa nchini Afghanitan na makamu
mwenyekiti wa Jirga Qiamuddin Kashaf amesema iwapo
watashindwa kufungua dirisha la amani kupitia mkutano huo wa jirga
hawataweza kufungua njia ya amani kwa mustakabali wa nchi hiyo.
Amesema wajumbe katika mkutano huo wameamua kuuufanya
mkutano huo uwe na mafanikio kwani hilo ndilo tamko lao, kwamba
hawataondoka katika mkutano huo wakiwa wameshindwa.
Waratibu wa mkutano, wamesema wajumbe katika mkutano huo,
waliitumia siku ya jana kwa kukaa katika makundi yapatayo 28,
kujadili ni nani Rais Hamid Karzai wa nchi hiyo anapaswa
kuwasiliana naye kwa mazungumzo ya amani na kwa vipi?.
Tayari wajumbe wameanza kuwasilisha mapendekezo yao katika
kikao cha leo kilichoanza mapema asubuhi, ambapo ndiyo siku ya
mwisho ya mkutano huo.
Wanadiplomasia wanasema kuwa makubaliano kama hayo ambayo
yameungwa mkono kwa kiasi kikubwa yatamuongezea haki rais
Karzai ya uongozi, wakati ambapo umaarufu wake kwa jamii ya
Waafghan uko chini huku serikali yake ikizingatiwa kuwa isiyofaa na
yenye rushwa.
Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan Staffan
de Mistura amesema mwaka huu ni mwaka wa Afghanistan
kufanikisha malengo yake hayo ama kuyaharibu.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani
Hilary Clinton amesema nchi yake inataka kupata taarifa kamili
kuhusiana na juhudi za Rais Karzai kuunganisha upya Taliban.
Mkutano huo mkubwa wenye lengo la kutatua tofauti na kuzungumzia
matatizo yanayoikabili jamii hiyo ya Waafghanistan unaojulikana
kama ''jigra'', ni sehemu muhimu katika ilani ya uchaguzi wa mwaka
jana katika kampeni za rais Karzai kuchaguliwa tena, ingawa awali
alisema kwamba hatazungumza na viongozi wa Taliban ambao wana
mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda au wale ambao
hawatataka kuacha mapigano.
Washirika wa magharibi wa Rais Karzai, hususan Marekani na
Jumuia ya Kujihami ya NATO wameelezea kuunga mkono mkutano
huo kama tukio muhimu la kihistoria katika kukomaa kisiasa kwa
Afghanistan baada ya kupinduliwa kwa utawala wa Taliban mwaka
2001.
Aidha Rais Karzai, ameahidi kuwapa nafasi za juu wapiganaji wa
Taliban na pia kuwapa msamaha watakapokubali kumaliza vita.
Hata hivyo kundi la Taliban limesema kwamba halitakubali
majadiliano mpaka pale majeshi yote ya kigeni yatakapoondoka
nchini humo.
Mwandishi: Halima Nyanza(afp)
Imepitiwa na: Hamidou Oummilkheir