Mkutano wa ajira ya vijana wa Ulaya mjini Paris
13 Novemba 2013"Muhimu zaidi ni kuharakisha" amesema rais Francois Hollande wa Ufaransa wakati wa mkutano pamoja na waandishi habari,mwishoni mwa mkutano huo wa kilele uliohudhuriwa na viongozi wote wa serikali na taifa wanachama wa Umoja wa Ulaya.
Francois Hollande aliyepania kuupindua mkondo wa vijana wanaosumbuliwa na ukosefu wa ajira,amesema mradi wa"Udhamini kwa vijana"unaotaja pasiwepo kijana wa Ulaya atakaesalia kwa muda wa miezi minne bila ya ajira,wala mafunzo,utaanza kutumika katika kipindi cha miaka miwili ijayo.
Lakini ili kuharakisha utaratibu wa kubuni nafasi za kazi kwa vijana "nchi zote zitakazokuwa tayari kuanzisha mradi huo zinaweza "kupatiwa fedha zinazohitajika kuanzia january mosi mwakani.
Kuhusu suala hilo mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya José Manuel Barroso amesema "njia muhimu za kupambana na ukosefu ajira miongoni mwa vijana zitategemea nchi wanachama.Panahitajika mipango thabiti na matukio ya haraka-amesema.
Mbinu ni tofauti
Kwa mujibu wa takwimu rasmi,mwezi september mwaka huu wa 2013,vijana milioni tano na laki nane wa Ulaya walisajiliwa hawana ajira:Ujerumani inayoangaliwa kama mfano mzuri wa nchi zinazopambana na ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana,asili mia 7.7 ya vijana hawana kazi katika wakati ambapo nchini Ufaransa idadi ya vijana wasiokuwa na kazi inafikia asili mia 25.Ugiriki na Hispania zimevunja rikodi,idadi ya vijana wasiokuwa na kazi katika nchi hizo inapundukia asili mia 56.
"BIla ya ukuaji wa kiuchumi,hakuna ajira kwa vijana.Siasa haibuni kazi,wajasiria mali ndio wanaobuni kazi-ameshadidia kansela Angela Merkel wa Ujerumani,aliyeitisha mkutano wa kwanza wa ajira kwa vijana mjini Berlin,July tatu iliyopita.
"Mwaka 2014 idadi ya wasiokuwa na kazi kwa bahati mbaya itasalia bado kuwa juu,lakini kuna ishara njema,kuna matumaini" amesema rais wa baraza la Ulaya,Herman Van Rompuy.
Euro bilioni 45 zimetengwa kupambana na ukosefu ajira
Nae spika wa bunge la Ulaya Martin Schulz anahisi mkutano huu wa kilele pekee ni ishara kwasababu viongozi wa taifa na serikali wamedhihirisha wanatilia maanani sana tatizo la ukosefu ajira miongoni mwa vijana.
Jumla ya Euro bilioni 45 zitatengwa katika kipindi cha miaka mitatu kugharimia miradi ya kubuni nafasi za kazi kwa vijana-Euro bilioni sita kati ya hizo zimetengwa na baraza la Ulaya tangu mwezi Juni uliopita.
Mwandishi:Hamidpou Oummilkheir/Reuters/AFP
Mhariri: Josephat Charo