1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Afrika na Umoja wa Ulaya, jee rais Mugabe ataalikwa ?

Mohammed Abdul-Rahman12 Julai 2007

Afrika kusini yasema hawezi kutengwa.

https://p.dw.com/p/CHB1

Uamuzi wa kumualika rais Robert Mugabe wa Zimbabwe katika mkutano wa kilele kati ya Afrika na Umoja wa ulaya mjini Lisbon, sasa utatolewa baada ya Ureno ikiwa mwenyekiti wa umoja wa ulaya kushauriana na wageni wengine kutoka Afrika.

Hali ya utata imezuka kuhusiana na kushiriki kwa Rais Mugabe kutokana na vikwazo vya usafiri katika nchi za umoja wa ulaya, vilivyoekwa na umoja huo dhidi ya maafisa wakuu kadhaa wa serikali ya Zimbabwe na chama tawala cha ZANU-PF akiwemo Mugabe.

Rais Mugabe amepigwa marufuku kusafiri katika nchi zote 27 za umoja wa ulaya, lakini balozi wa Ureno nchini Afrika kusini hakuondoa uwezekano wa nchi yake ikiwa mwenyekiti wa sasa wa umoja huo, kumruhusu kiongozi huyo wa Zimbabwe mwenye umri wa miaka 83 ashiriki katika mkutano wa kilele wa Lisbon mwezi Desemba.

Vikwazo hivyo vimetokana na madai ya kufanyika mizengwe katika uchaguzi wa rais wa 2002, lakini kiongozi huyo anaishitumu Uingereza kwa kuongoza kampeni hiyo, kwa kile alichokisema ni kutokana nna uamuzi wa serikali yake kuyatwaa mashamba ya wazungu kuyagawa kwa waafrika wasio na ardhi. Hata hivyo wakosoaji wake wanasema mashamba hayo yamegawanywa kwa vigogo wa serikali na chama tawala Zanu-Pf.

Balozi wa Ureno nchini Afrika kusini Paulo Barbosa alisema mjini Johannesburg kwamba kwa wakati huu wanazingatia utaratibu wa kumualika Mugabe pamoja na viongozi wengi wa Afrika. Balozi huyo alikua akifafanua juu ya mipango ya Ureno kuhusu Afrika katika kipindi chake cha miezi sita ikiwa .Mwenyekiti wa umoja wa Ulaya.

Barbosa alisema kinachozingatiwa hivi sasa ni masuala ya kujadiliwa wakati wa mkutano huo, kama vile uhamiaji na mabadiliko ya hali ya hewa, katika hali itakayoyafaidisha mabara yote mawili.

Baadhi ya nchi za kiafrika zimekua zikisisitiza kwamba zitalazimika kuzingatia upya kushiriki kwao, ikiwa Mugabe atatengwa , matamshi ambayo yametishia kuutia dosari mkutano huo. Msimamo huo ulidhihirika tena wiki iliopita, pale Waziri mdogo wa mambo ya nchi za nje wa Afrika kusini Aziz Pahad aliposema kwamba Afrika haitoiruhusu Ulaya imtenge Mugabe katika mkutano huo kati ya bara hilo na umoja wa ulaya.

Katika mahojiano, Bw Pahad alisema Afrika haitokubali ipangiwe nani awemo na nani asiwemo katika ujumbe wake, kwani alisema leo ni Zimbabwe na kesho inaweza kuwa ni sisi akimaanisha Afrika kusini au nchi nyengine.