1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano muhimu wa NATO waanza Warsaw

Admin.WagnerD8 Julai 2016

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameitetea mipango ya mfungamano wa kijeshi wa NATO ya kuongeza idadi ya wanajeshi katika Ulaya ya kati na ya mashariki kutokana na mivutano na Urusi.

https://p.dw.com/p/1JLZB
Jenerali wa Marekani Frederick B. Hodges, kamanda wa NATO barani Ulaya
Jenerali wa Marekani Frederick B. Hodges, kamanda wa NATO barani UlayaPicha: picture alliance/dpa/T. Zmijewski

Kansela Merkel ameilaumu Urusi kwa kuchukua hatua zinazosababisha kupotea kwa hali ya kuaminiana. Kiongozi huyo wa Ujerumani ameyasema hayo kabla ya kuanza kwa mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi za NATO mjini Warsaw.

Merkel amesema Nato inahitaji kuimarisha uwepo wake katika maeneo ya Baltiki na Poland.

Akihutubia bungeni kutoa tamko la serikali, juu ya NATO, bibi Merkel alisema Ujerumani itachangia kwa kiwango kikubwa katika utekelezaji wa mipango ya jumuiya hiyo ya kuweka idadi kubwa ya wanajeshi katika Ulaya ya mashariki.

Akiitetea mipango hiyo kiongozi huyo wa Ujerumani ameeleza kwamba viongozi wa nchi za mfungamano wa kijeshi wa NATO wanakutana mjini Warsaw wakati ambapo hali ya usalama imebadilika sana barani Ulaya.

Amesema katika Ulaya ya mashariki Urusi imechukua hatua zilizowatikisa sana washirika wa NATO.

Kansela Merkel amesema ikiwa kanuni ya kuheshimu uhuru na mipaka ya nchi inakiukwa kwa kauli na matendo,hali ya kuaminiana inapotea.

Na kutokana na hali hiyo amesema jumuiya ya NATO inapaswa kuwapa uhakika washirika wake wa Ulaya ya mashariki.

Viongozi kutoka nchi 28 za jumuiya hiyo wanatarajiwa kukubaliana kwenye mazungumzo yao ya siku mbili, katika mji mkuu wa Poland Warsaw, juu ya hatua ya kuongeza vikosi vya wanajeshi hadi 1000 nchini Poland.

Mdahalo na Urusi ni muhimu

Hata hivyo Kansela Merkel amesisitiza umuhimu wa kuendeleza mdahalo na Urusi licha ya kuilaumu nchi hiyo kwa kuchukua hatua zinazosababisha hali ya wasi wasi.

Vifaru vya Ujerumani, aina ya Leopard
Vifaru vya Ujerumani, aina ya LeopardPicha: Getty Images/AFP/C. Stache

Wakati huo huo Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry amewasili nchini Ukraine kwa lengo la kuihakikishia nchi hiyo kwamba Marekani itasimama pamoja nayo katika kuitatua mizozo yake ya mipaka na Urusi.

Lakini balozi wa Urusi katika NATO,Alexander Grushko ameilaumu jumuiya ya NATO kwa kuendesha siasa ya mvutano na amezionya nchi za jumuiya hiyo kuwa Urusi itachukua hatua za kuikabili sera hiyo. Balozi Grushko ameliambia gazeti la "Kommersant" la nchini Urusi kwamba NATO inapaswa kuelewa kuwa hatua inazochukua hazitaleta tija kijeshi.

Kwenye mkutano wao mjini Warsaw viongozi wa NATO wanatarajiwa kusisitiza dhamira ya kuwalinda washirika wote wa jumuiya hiyo.

Nchi za Ulaya mashariki ambazo ni wanachama wa NATO, ikiwa pamoja la Poland zimeingiwa wasi wasi tangu Urusi iliteke jimbo la Crimea la Ukraine.Viongozi wa NATO pia wataijadili hali ya nchini Afghanistan inayozidi kuzorota.

Mwandishi:Mtullya abdu/dpa,afp

Mhariri:Iddi Ssessanga