Mkutano mkuu wa ZANU-PF waanza
2 Desemba 2014Katika mkutano huo, rais Robert Mugabe wa Zimbabwe anatarajiwa kuchaguliwa tena kuwa mwenyekiti wa chama. Pamoja na hayo ZANU-PF inatarajiwa kupitisha mabadiliko ya katiba yake ili kumruhusu Mugabe kuwachagua manaibu wake moja kwa moja. Hatua hiyo itaongeza madaraka ya kiongozi huyo mkongwe mwenye miaka 90 sasa. Hata hivyo, mkutano huu unafanyika wakati kukiwa na mvutano wa madaraka ndani ya chama. Wachambuzi wa kisiasa wanaamini kwamba wapo viongozi wengi wa juu watakaopoteza nafasi zao.
Wiki iliyopita makamu wa rais wa Zimbabwe Joyce Mujuru alinyang'anywa nyadhifa zake katika chama tawala. Mujuru mwenye miaka 59 pamoja na waziri wa sheria Emmerson Mnangagwa walikuwa miongoni mwa wanachama wa ZANU-PF waliokuwa wakiwania kuchukua kiti cha Mugabe ambaye amekuwa rais wa Zimbabwe tangu nchi hiyo ilipopata uhuru mwaka 1980. Hata hivyo, Mujuru alijikuta kwenye kashfa baada ya Grace Mugabe, ambaye ni mke wa rais, kudai kwamba Mujuru alikuwa amepanga njama ya kumuua rais. Pamoja na hayo, Grace Mugabe alimshutumu Mujuru kwa kula rushwa na kuleta mgawanyiko ndani ya chama tawala.
Grace Mugabe kumrithi mume wake?
Grace Mugabe aliwashangaza wengi awali mwaka huu alipochaguliwa kuongoza idara ya wanawake ya ZANU-PF. Kabla ya hapo, alikuwa amejipatia shahada ya uzamifu katika chuo kikuu kimoja cha Zimbabwe lakini cha ajabu ni kwamba aliipata shahada hiyo miezi michache tu baada ya kujiunga na chuo hicho. Robert Mugabe ameutetea uteuzi wa mke wake kuiongoza idara ya wanawake na inaaminika kwamba Grace Mugabe anaandaliwa kuichukua nafasi ya mume wake ikulu.
Mwanasiasa mwingine anayepewa nafasi kubwa ya kuchukua nafasi ya Mugabe ni waziri wa sheria Mnangagwa. Waziri huyo alikuwa miongoni mwa wapiganaji walioongoza mapambano ya kudai uhuru katika miaka ya 1970. Baada ya Zimbabwe kupata uhuru mwaka 1980, Mnangagwa aliteuliwa kuwa waziri wa ulinzi. Tangu wakati huo ameongoza wizara mbali mbali ikiwemo ya fedha na ile ya makazi.
Mwandishi: Elizabeth Shoo/afp
Mhariri: Josephat Charo