1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano mkuu wa wawakilishi wa umma mjini Beijing

5 Machi 2012

Waziri mkuu wa China Wen Jiabao afungua mkutano mkuu wa umma katika wakati ambapo China inajiandaa kukabiliana na changamoto mpya.

https://p.dw.com/p/14FMW
Kasri mkutano mkuu wa Umma unakofanyikaPicha: dapd

Ukuaji hafifu wa kiuchumi,huduma madhubuti kwa jamii za mashambani na kujiimarisha kijeshi,ndizo mada zilizoshadidiwa na waziri mkuu wa China Wen Jiabao katika hotuba yake mbele ya wawakilishi wanaohudhuria mkutano mkuu wa umma mjini Beijing.Mkutano wa mwaka huu unagubikwa pia  na mitihani inayotokana na matatizo ya kiuchumi duniani,lawama za wakulima na uhasama miongoni mwa nchi za Asia.

Katika hotuba yake kuhusu siasa jumla mbele ya wajumbe wanaohudhuria mkutano mkuu wa umma,waliojazana katika kasri la umma mjini Beijing,waziri mkuu Wen Jiabao amechambua kwa muda wa saa mbili changamoto zinazoikabili China katika wakati ambapo nchi hiyo inajiandaa kuwakaribisha viongozi wepya.

Akitilia maanani mgogoro wa fedha unaoendelea barani Ulaya,na ukuaji hafifu wa kiuchumi nchini Marekani-washirika wake wawili wakubwa,China nguvu ya pili muhimu ya kiuchumi ulimwenguni,imepunguza lengo la ukuaji wake wa kiuchumi kwa mwaka huu na kusalia asili mia 7.5 dhidi ya asili mia 8 mwaka jana.

Wadadisai wa kiuchumi wanahisi wakati umepita ambapo China iliweza kuona pato la ndani likikuwa kwa asili mia 10.04 kama ilivyotokea mwaka 2010.Baada ya kufikia asili mia 9.2 mwaka jana ukuaji wa kiuchumi unategemewa kupungua kidogo mwaka huu na kufikia asili mia 8 hadi asili mia 8.5.

Wen Jiabao, Eröfnung des Chinesischen Volkskongresses in Peking
Waziri mkuu Wen Jiabao, akihutubia wajumbe mkutanoniPicha: Reuters

Akihutubia mbele ya wawakilishi elfu tatu waliokuwa wakisikiliza kwa makini, wengine wamevalia kijeshi na baadhi suti za kiasili,waziri mkuu Wen Jiabao amedhibitisha azma ya Beijing ya kuanzisha mageuzi ya kiuchumi kwa kupunguza mzigo wa mashirika yanayomilikiwa na serikali.

China inapanga kumalizana na mtindo wa kumiliki peke yake mashirika ya umma na badala yake kuhimiza wawekezaji wa kibinafsi katika sekta ya reli,shughuli za fedha,nishati,mawasiliano,elimu na huduma za afya-amesema hayo waziri mkuu Wen akigusia mapendekezo ya hivi karibuni ya benki kuu ya dunia.

Akitupia jicho mkutano mkuu wa chama cha kikoministi unaotarajiwa kuwateuwa viongozi wepya mwezi October mwaka huu,waziri mkuu Wen Jiabao amezungumzia umuhimu wa amani katika jamii na hasa mashambani ambako sauti zinazidi kupazwa dhidi ya watu kupokonywa ardhi kwa njia za kimabavu.

"Haki ya wakulima katika ardhi wanayoilima,ambako nyumba zao zinakutikana ni haki ambazo hakuna anaeweza kuzivunja."

Waziri mkuu ameahidi pia utawala "safi" na adhabu kali kwa wote wanaopokea rushwa.

China / Militär / Peking
Wanajeshi ni miongoni mwa wanaohudhuria mkutano huo mkuuPicha: Reuters

Kwa upande wa kijeshi China inapanga kuligeuza jeshi lake liwe la kimambo leo.Bajeti ya jeshi itaongezeka kwa asili mia 11.2 mwaka huu.

"Tutaimarisha nguvu zetu za kijeshi kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano."Amesema waziri mkuu Wen Jiabao.

Matamshi hayo yanaweza kuzidisha hofu ya Marekani iliyotangaza azma ya kurejea katika eneo la Asia-Pacific na pia majirani wa China wanaohofia Beijing isije ikataka kujiingiza katika mizozo ya kupigania mamlaka ya baharini katika eneo hilo.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Afp

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman