1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Gauck asifu mchango wa kanisa

26 Mei 2016

Wakatoliki wameanza mkutano wao mkuu wa mia moja katika mji wa Leipzig. Wajumbe kwenye mkutano huo pamoja na masuala ya kidini wanazumguzia juu ya mgogoro wa wakimbizi na haki za wanawake makazini

https://p.dw.com/p/1IubE
Rais wa Ujerumani Joachim Gauck mjini Leipzig
Rais wa Ujerumani Joachim Gauck mjini LeipzigPicha: picture-alliance/dpa/J. Woitas

Mkutano wa Wakatoliki mjini Leipzig ulianza kwa ujumbe wa video wa Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis.

Baba Mtakatifu amewataka Wakatoliki waishi kwa amani na washikamane na watu wazima,wagonjwa na wakimbizi. Pia amewataka wakatoliki wauzingatie umuhimu wa kuyalinda mazingira.

Maalfu ya Wakatoliki, pamoja na Rais wa Ujerumani Joachim Gauck walihudhuria sherehe za ufunguzi wa mkutano huo mkuu wa Mia moja wa Wakatoliki,unaoendelea mjini Leipzig, mashariki mwa Ujerumani.

Bwana Gauck ambae hapo awali alikuwa kasisi wa kanisa la kiprotestanti katika Ujerumani Mashariki, ameusifu mchango unaotolewa na kanisa nchini Ujerumani. Ametoa shukurani kwa niaba ya jamii na serikali, kwa mchango huo unaotolewa na Wakatoliki na Wakrsito wa madhehebu mengine. Ametilia maanani moyo wa mshikamano ulioonekana wazi katika kuwapokea wakimbizi, mnamo miezi ya hivi karibuni.

Rais wa Ujerumani pia alisisitiza juu ya uhuru wa kuabudu.Ameseama kutokana uhuru wa dini kuwa haki ya kimsingi, unalindwa na serikali.

Hapo awali Mwenyekiti wa kamati kuu ya Wakatoliki wa Ujerumani Thomas Sternberg aliahidi kufanyika mkutano huo kwa ajili ya watu wote, chini ya kaulimbiu inayosema "oneni pale yuko mwanadamu, njooni nyote pamoja, waumini na msiokuwa waumini."

Mwenyekiti huyo amekumbusha kwamba Ujerumani Mashariki ambako mkutano wa wakatoliki unafanyika ni eneo mojawapo ,barani Ulaya,lililopo mbali na kanisa na kwa sababu hiyo ,amesema ni muhimu kwa Wakatoliki kujitokeza na kuzigusa nyoyo za wote kwa urafiki na unyenyekevu .

Stahamala ndio lakini AfD hapana

Hata hivyo mhashamu Sternberg amesisitiza msimamo wake juu ya kutowaalika wajumbe kutoka chama cha mrengo wa kulia, cha wapinga Ulaya na wahamiaji ,AfD Mwenyekiti huyo wa kamati kuu ya wakatoliki wa Ujerumani ameeleza kwamba mkutano wa mjini Leipzig unapaswa utoe ishara ya stahamala.

Wajumbe kwenye mkutano wa Wakatoliki mjini Leipzig
Wajumbe kwenye mkutano wa Wakatoliki mjini LeipzigPicha: picture-alliance/dpa/J. Woitas

Mji wa Leipzig ambako mkutano wa wakatoliki unafanyika una wakaazi wapatao 570,000 na kati ya hao ni asilimia 4,3 tu ambao ni Wakatoliki.

Na aliekuwa Rais wa Ujerumani Christian Wulff pia anahudhuria mkutano wa mjini Leipzig. Katika hotuba yake aliishutumu jumuiya ya wapinga Uislamu na wahamiaji ,ya Pegida. Bwana Wulff ameuliza jee Ujerumani imefikia wapi?

Wajumbe wa kudumu zaidi ya 32,000 wanatarajiwa kushiriki kwenye mkutano wa mjini Leipzig. Spika wa Bunge la Ujerumani,Nobert Lammert,Waziri wa mambo ya ndani Thomas de Maiziere na Makamu wa Kansela Sigmar Gabriel pia watahudhuria mkutano huo siku ya Jumamosi.

Mwandishi:Mtullya abdu./dpa,afpe

Mhariri: Josephat Charo