1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano mkuu wa die Grüne Magazetini

24 Novemba 2014

Mkutano mkuu wa chama cha walinzi wa mazingira die Grüne mjini Hamburg,hali nchini Afghanistan na matumizi ya nguvu dhidi ya wanawake ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/1Ds5m
Kitambulisho cha msimamo wa kupendelea amani miongoni mwa walinzi wa mazingira die Grüne nchini UjerumaniPicha: picture-alliance/dpa/Jens Büttner

Tuanzie Hamburg ambako walinzi wa mazingira die Grüne walikuwa na mkutano wao mkuu.Mengi yaliyofikiriwa yangetokea kutokana na mivutano ya ndani chamani,hayakushuhudiwa.Gazeti la "Reutlinger General-Anzeiger" linaandika:

Mkutano mkuu wa kubuni mwongozo,malumbano kati ya makundi ya nadharia tofauti chamani au hata hofu ya kuzuka machafuko ndio sura iliyojitokeza kabla ya mkutano mkuu wa Hamburg kuitishwa.Eti kuna lililotokea?Hasha,hata kidogo.Wajumbe wamejadiliana na baadhi ya wakati kufika hadi hata ya kuzozana,lakini hakujakuwa na la ziada.Kwasababu hata uongozi wa chama hivi sasa umebadilika,na mafundo yaliyokuwepo yamelainishwa.

Hata hivyo gazeti la "Rhein-Zeitung" linahisi mengi yameachwa kando badala ya kujadiliwa.Gazeti linaendelea kuandika:

Mada zinazozusha mabishano kati ya wale wanaojiita Realo-au wanaofuata hali halisi ya mambo namna ilivyo na wenzao wanaoelemea zaidi mrengo wa shoto chamani zimeepukwa kwa hivyo zinaweza haraka kuibuka.Mada kuhusu malipo ya kodi kwa mfano haikujadiliwa.Wafuasi wa mrengo wa shoto wanapigania kodi ya mapato izidishwe kwa wale wanaojimudu na matajiri,wenzao wa Realo wanaopigania msimamo wa tahadhari wakikumbusha uchaguzi mkuu wa mwaka 2017.Katika daraja ya shirikisho,walinzi wa mazingira wanalenga kuunda serikali ya muungano pamoja na vyama ndugu vya kihafidhina vya CDU/CSU.Kwakuwa muungano wa vyama vitatu vya mrengo wa shoto-yaani SPD,walinzi wa mazingira die Grüne na wafuasi wa chama cha die Linke haupewi nafasi nzuri ya kufanikiwa katika daraja ya shirikisho-muungano pamoja na CDU/CSU ndio unaoangaliwa na walinzi wa mazingira kama njia ya kurejea tena madarakani baada ya uchaguzi wa mwaka 2017.

Jinamizi la Iraq liepukwe Afghanistan

Hali nchini Afghanistan imemulikwa pia na wahariri wa magazeti ya Ujerumani wakikumbusha muda unakurubia wa vikosi vya kimataifa vinavyoongozwa na jumuia ya kujihami ya NATO kuihama nchi hiyo.Gazeti la "Leipziger Volkszeitung" linaandika:

Ukurasa wa Afghanistan bado hauwezi kufungwa,kama zinavyopendelea nchi za magharibi.Hali katika nchi hiyo haiyendi kuambatana na maamuzi yanayopitishwa bungeni mjini Berlin au Washington.Shambulio la mwishoni mwa wiki ni ushahidi mwengine wa kusikitisha wa matumzi ya nguvu ya kinyama kabisa yanayowasumbuwa wakaazi wa nchi hiyo.Rais Barack Obama wa Marekani ameanza kugutuka.Vikosi vitakavyosalia vya Marekani vinabidi vipatiwe fursa kubwa zaidi ya kuwajibika.Mshindi huyo wa tuzo ya amani ya Nobel analikumbuka bila ya shaka jinamizi la Iraq.Muda mfupi baada ya vikosi vya Marekani kuihama nchi hiyo,wafuasi wa itikadi kali wa dola la kiislam wakaanza kujieneza.Bado si dhahir mwelekeo huu mpya Marekani utajibiwa vipi na nchi shirika.Pengine jeshi la Ujerumani Bundeswehr likatakiwa pia libadilishe mipango yake.

Siku ya Umoja wa Mataifa dhidi ya Matumizi ya Nguvu dhidi ya Akinamama

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu matumizi ya nguvu dhidi ya akinamama.Gazeti la "Mittelbayerische Zeitung" linaandika:

Fuko la Umoja wa mataifa la Maendeleo ya akinamama linakadiria katika baadhi ya nchi asili mia hadi 70 ya akinamama wamewahi anglao mara moja maishani mwao kuangukia mhanga wa matumizi ya nguvu,kimwili au kingono.Mara nyingi visa hivyo hujiri kupitia mtu wa karibu sana na famila.Siku ya kimataifa ya kupambana na matumzi ya nguvu dhidi ya wanawake itafichua hapo kesho madhila wanayokumbana nayo akina mama.Na hilo ni muhimu kupita kiasi.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Yusuf Saumu