Mkutano mkuu wa Chama cha SPD cha Ujerumani umemalizika
16 Novemba 2009Jana mjini Dresden ulimalizika mkutano mkuu wa Chama cha Social Democratic, SPD, cha hapa Ujerumani. Ulifanyika kama alama ya kushindwa kukubwa, jambo ambalo halijawahi kutokea katika historia yake, kwa chama hicho katika uchaguzi mkuu uliopita. Mkuu wa chama hicho, Sigmar Gabriel, alizungumzia juu ya chimbuko na mwanzo mpya kwa chama hicho.
Zilikuwa siku tatu zilizojaa majadiliano, siku tatu ambapo wajumbe wa mkutano walitoa joto lao, siku tatu ambapo kwamba mielekeo ya Chama cha SPD ilipangwa upya. Hakujakosekana lawama kali dhidi ya njia iliopita chama hicho katika miaka kumi na moja iliopita. Mjumbe wa kutoka mkoa wa Bayern, Harald Unfried, aliwazungumzia watu wengi pale aliposema hivi katika mkutano mkuu:
" Nje, katika nchi, hakujawahi kuweko watu wengi waliounga mkono wafanya kazi wastaafu wakiwa na umri wa miaka 67, hakujawahi kuweko na wingi wa watu waliounga mkono msaada kwa watu waziojiweza usukwe chini ya mfumo wa Hartz Nambari nne, hakujakuweko watu wengi waliounga mkono kubinafsishwa shirika la reli la Ujerumani, hakuna wingi hivi sasa wa watu wanaouunga mkono kuweko jeshi la Ujerumani huko Afghanistan, hakujakuweko na wingi watu waliounga mkono kupanuliwa mfumo wa watu kuajiriwa na kampuni ambazo ni wakala wa kampuni zinazotafuta wafanya kazi, hayo ni mambo ambayo sisi tumeingizwa ndani yake."
Baada ya majadiliano marefu, wajumbe wa mkutano waliuunga mkono mswaada wa azimio lilotolewa na uongozi wa chama. Ndani ya mswaada huo kulitolewa samahani nyingi kutokana na mambo yaliotendeka miaka iliopita, ile sheria ya kuwafanya wafanya kazi wastaafu wakiwa na umri wa miaka 67 iliwekewa alama ya kuuliza. Kinyume na ulivotaka uongozi, mkutano mkuu huo pia ulipitisha azimio la kurejeshwa tena kodi ya kuwatoza wenye kumiliki mali nyingi. jambo hilo lilishikiliwa sana na kiongozi wa tawi la vijana la Chama cha SPD, Juso, Franziska Drohsel.
Sio tu maelezo ya mielekeo mipya ilitajwa. Pia Chama cha SPD kimejipanga upya linapokuja suala la viongozi wake. Aliyekuwa zamani waziri wa mazingira, Sigmar Gbariel, baada ya kutoa hotuba yake ya kusisimua ya muda wa saa mbili, alichaguliwa kwa wingi mkubwa kuwa mkuu mpya wa chama. Pamoja na katibu mkuu mpya, Andrea Nahles, yeye, Gabriel, anataka kuweko demokrasia zaidi ndani ya chama, maamuzi yachukuliwe kutoka ngazi za chini kwenda juu chamani. Jumuiya zote za chama hicho, kutoka uongozi wa shirikisho wa chama hicho hadi katika mashina ya chama, sauti za wanachama lazima zisikilizwe:
" Ndio maana mimi naunga mkono kwamba kila mwaka tuwe na mkutano mkuu, kwa vile sisi hatupigi kura, basi sisi tutazungumza juu ya siasa na watakaoamuwa ni nyinyi; hali hiyo tunaitaka tukiwa upande wa upinzani."
Pia mkuu wa wabunge wa Chama cha SPD, Frank Walter Steinmeier, aliahidi kwamba atawakilisha siasa kali za upinzani bungeni:
"Tuelekee kwenye kazi, tuangalie mbele, tusiwachie wengine, serekali hii ya vyama vya CDU/CSU na FDP, tusiiache ikapumua katik wiki zijazo."
Katika siku ya mwisho ya mkutano mkuu huo, Erhard Eppler, mwenye umri wa miaka 82, aliwahutubia wajumbe. Yeye alikuweko katika mkutano mkuu kama huu, miaka 50 iliopita, wakati ule mwongozo wa Chama cha SPD, uliopewa jina la Mpango wa Godesberg, ulipokubaliwa. Kutoka hapo chama hicho kilijigeuza kutoka kuwa chama cha wafanya kazi na kuwa chama cha umma. Alisema tamko muhimu la mpango huo lazima leo pia litajwe, nalo:
"Uhuru na haki ni vitu vinafungamana, na katika mambo hayo ndipo ilipo falsafa yote ya demokrasia ya kijamii. Katika tamko hilo dogo tunaamini kwamba haki zaidi inamaanisha uhuru zaidi."
Mwakani Chamna cha SPD kitakuwa na mkutano mkuu mwengine ambapo kitaendelea kuzungumzia juu ya siasa zake.
Mwandishi:Berrina Marx/ZR / Othman Miraji
Mhariri:M.Abdul-Rahman