Mkutano kujadili ujenzi mpya wa Somalia
21 Mei 2010Mkutano huo, unafanywa mjini Istanbul Uturuki kuanzia leo tarehe 21 -hadi 23 Mei kutafuta njia ya kuisaidia Somalia ambayo tangu takriban miaka ishirini iliyopita,inajikuta katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Serikali ya mpito ya Rais Sheikh Sharif Sheikh Ahmed inaungwa mkono na jumuiya ya kimataifa lakini nyumbani haina ushawishi mkubwa hivyo kama anavyoeleza mwandishi wa habari wa Somalia, Shidane Dabaan.
"Serikali inadhibiti eneo la kilomita tano tu, katika nchi nzima, yaani barabara inayotokea makao rasmi ya rais na kuelekea uwanja wa ndege."
Mkutano wa Umoja wa Mataifa nchini Uturuki utajadili njia za kuisaidia Somalia na kuijenga upya nchi iliyoteketezwa kwa vita. Katika miezi iliyopita,nchi hiyo mara nyingi, ilikuwa ikitajwa pale meli ya mizigo iliyotokea Ulaya au Marekani ilipotekwa nyara mbele ya pwani yake. Lakini maharamia hao sio kitisho kikubwa kutoka nchi hiyo ya Pembe ya Afrika, bali ni makundi ya Kiislamu yaliyodhibiti takriban maeneo yote nchi. Kundi mojawapo ni Al-Shabaab linalosema kinagaubaga kuwa linashirikiana na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda.
Hata Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton alipokuwa ziarani Afrika ya Mashariki hivi karibuni,alieleza waziwazi maoni yake kwamba Somalia sasa imekuwa kambi mpya ya makundi ya kigaidi na kuongezea:
"Marekani inatia maanani vitisho vinavyosababishwa na Al Shabaab hasa kwa watu wa Somalia na nchi za jirani pia kama vile Kenya."
Waziri Clinton amesema, kwa mujibu wa habari walizopokea, Al Shabaab hawatumii tu wapiganaji na fedha kutoka nje bali hata mipango ya kuwashambulia watu wa Somalia.
Hadi sasa jitahada zote za kuunda serikali imara nchini Somalia hazikufanikiwa. Serikali ya hivi sasa ni dhaifu kabisa. Rais Ahmed alieshika madaraka kama mwaka mmoja uliopita na alietumainiwa kurejesha amani na utulivu Somalia,bado hajafanikiwa kupatanisha makundi mbali mbali nchini humo.
Hata hivyo, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Somalia,Ahmedou Ould- Abdallah anaamini njia pekee iliyopo ni kuwapiga vita wanamgambo wa Kiislamu na kuiunga mkono serikali ya mpito ili utulivu wa aina fulani uweze kupatikana. Amesema watu wenye njaa ni wahanga wa wanamgambo na wanapaswa kukombolewa.
Hivi karibuni tu shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi, lilionya kuwa idadi ya Wasomali waliopoteza makaazi yao huenda ikaongezeka. Hivi sasa kiasi ya watu milioni moja na laki nne wamekimbia makwao na idadi hiyo huenda ikaongezeka kwa laki tatu wengine na haijulikani pa kuwapeleka. Kambi zilizo mpakani na Kenya zimeshajaa.
Mwandishi:Diekhans,Antje/ZPR/P.Martin
Mhariri: M.Abdul-Rahman