Mkutano wa usalama waanza Munich
16 Februari 2018Katibu Mkuu wa Jumuiya ya kujihami ya NATO Jens Stoltenburg, alisema jumuiya hiyo inaongeza juhudi za kuvitayarisha vikosi vyake kuikabili Urusi katika eneo la Baltic lakini akaonya dhidi ya kuanzisha vita vipya baridi au mashindano ya silaha. Akizungumza mjini Munich Stoltenberg alisema wanaendelea kufuatilia mdahalo na Urusi.
Miongoni mwa mada muhimu zinazojadiliwa katika mkutano huo wa usalama ni michango ya fedha ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kwa jumuiya ya NATO huku Marekani na NATO zikipendelea Ujerumani iongeze mchango wake. Stoltenberg alisema bila shaka baada ya miaka 20 ya kubana matumizi katika ulinzi Ujerumani na nchi nyingine nyingi washirika wa NATO, kuna mapungufu.
"Lakini hii ndio sababu kwa nini ni muhimu kwamba Ujerumani na washirika wote wa NATO wameanza kuwekeza zaidi katika ulinzi. Tunaipongeza Ujerumani kwa yale inayoyafanya, lakini tunashukuru kwamba itafanya mengi zaidi."
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen aliahidi Ujerumani itatumia fedha zaidi katika jeshi lake na michango kwa Umoja wa Mataifa, lakini akayataka mataifa mengine yaendelee kujishirikisha. Aliikosoa Marekani kwa kupunguza utoaji misaada ya kigeni na michango kwa Umoja wa Mataifa.
Waziri von der Leyen na waziri wa ulinzi wa Ufaransa, Florence Parly walisema nchi za Ulaya zinahitaji kuhakikisha zina uhuru wa kimkakati kujibu vitisho vya usalama, hata zinapoimarisha michango yao kwa jumuiya ya NATO.
Wakizungumza katika mkutano wa Munich, wamaziri hao walisisitiza Ulaya lazima iweze kujisimamia yenyewe katika masuala ya ulinzi.
Usalama waimarishwa
Usalama umeimarishwa mjini Munich huku maafisa 4000 wa polisi wakitumwa kupiga doria katika mkutano huo unaoanza leo hadi siku ya Jumapili. Mwenyekiti wa mkutano wa usalama wa Munich, Wolfgang Ischinger, alisema kuna masuala mengi nyeti yanayotakiwa kujadiliwa ikiwemo pia mizozo, hofu ya machafuko kuongezeka na kuyumba kwa hali ya kisiasa.
Ischinger alisema, "Natumai mkutano wa Munich unaweza kutoa mchango katika kuanza tena kwa aina fulani ya mazungumzo, sio tu kati ya Urusi na Marekani, bali pia kati ya Urusi na mataifa mengine muhimu, kwa mfano Ukraine. Nina matumaini, lakini lazima tuwe wakweli. Kwa sasa tuko katika hali mbaya tukizingatia usalama wa dunia."
Marekani inawaskilishwa na jenerali Herbert Raymond Mcmaster, ambaye amekuwa mshauri wa usalama wa taifa wa rais Donald Trump kwa mwaka mmoja uliopita, pamoja na waziri wa ulinzi Jim Mattis, ambaye ni jenerali mstaafu.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alikutana na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres mjini Munich, huku Iran ikiwakilishwa na waziri wake wa mambo ya nchi za nje wa Iran, Javad Zarif, katika mkutano huo.
Waziri wa muda mrefu wa mashauri ya nchi za kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov, ni mshirika muhimu katika mkutano unaosubiriwa kwa hamu kubwa na mwenzake wa Ujerumani, Ufaransa na Ukraine kujadili mzozo mashariki ya Ukraine. Mkutano huo uliopangwa kufanyika baadaye leo kandoni mwa mkutano wa Munich, ni wa kwanza wa aina yake wa ule mfumo wa Normandy katika kipindi cha mwaka mmoja, kutathmini jinsi mzozo wa Ukraine ulivyoachiwa kuendelea kutokota.
Mwandishi:Josephat Charo/dpae
Mhariri:Saumu Yusuf