Mkutano kuhusu Mashariki ya Kati waingia siku ya pili
14 Februari 2019Kuelekea mkutano huo Netanyahu alitoa ujumbe kupitia mkanda wa vidio uliowekwa ukurasa wa Twitter akisema kwamba, mataifa ya kiarabu yanayohudhuria mkutano huo yana maslahi ya pamoja na Israel katika vita dhidi ya Iran.
Waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammed Javad Zarif alimjibu kiongozi huyo akisema "siku zote tumefahamu fikra za uwongo za Netanyahu. Na sasa ulimwengu mzima unaohudhuria mkutano wa Warsaw umefahamu hilo."
Vidio hiyo ambayo iliwekwa na ofisi ya Netanyahu imefutwa katika mtandao wa twitter na baadae Netanyahu alisema kuhudhuria mkutano huo ni "hatua ya kihistoria". Netanyahu ni mshiriki katika mkutano huo uliondaliwa na Marekani na Poland kujaribu kusaka amani na usalama katika eneo la mashariki ya Kati. Lakini hadi sasa kumekuwa na idadi ndogo ya washiriki huku nchi kadhaa za barani Ulaya zikituma maafisa wa ngazi ya chini na ukosoaji kwamba uliilenga Iran.
Mataifa hayo yanaikosoa Marekani kwa kujiondoa mkataba wa kimataifa wa nyuklia na Iran na kujaribu kuyasaidia makampuni ya Ulaya yanayofanya biashara na Iran kuepuka athari za vikwazo vya Marekani.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo amesema wanatafuta zama mpya za ushirikiano katika Mashariki ya Kati. Iran na Urusi zimekataa kuhudhuria huku Rais Vladmir Putin akiitisha mkutano mwingine kwenye mji wa kitalii wa Sochi sambamba na rais Hassan Rouhani wa Iran na mwenzao wa Uturuki Recep Tayyip Erdogn.
Iran imelaani mkutano huo ikisema ni jaribio la Marekani kushinikiza maamuzi yake ya kisera. Maafisa wa Marekani walisisitiza kuwa Iran sio mlengwa katika mkutano huo. Washington mara kadhaa imeituhumu Tehran kwa kuwa na sera za kudhoofisha mataifa ya kanda ya Mashariki ya Kati na kufadhili ugaidi. Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas ni miongoni mwa mawaziri wa kigeni wa magharibi aliyejiondoa kushiriki.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP/dpa
Mhariri: Iddi Ssessanga