1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa wamalizika mjini Washington

Josephat Charo16 Februari 2007

Mkutano kuhusu ongezeko la joto duniani ulimalizika jana mjini Washington, Marekani. Viongozi kutoka mataifa 13 walitia saini taarifa ya pamoja kuzishinikiza serikali zao ziunde kwa haraka mpango wa kupunguza gesi zinazotoka viwandani, kabla mkataba wa Kyoto kumalizika ifikapo mwaka wa 2012.

https://p.dw.com/p/CHJz
Moshi kutoka viwandani unasababisha ongezeko la joto duniani.
Moshi kutoka viwandani unasababisha ongezeko la joto duniani.Picha: AP

Viongozi kutoka mataifa 13 walimaliza mkutano wao kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa duniani mjini Washington hapo jana. Mkutano huo ulizungumzia pia suluhisho la muda mrefu kwa ongezeko la joto duniani. Viongozi hao walitoa mwito kuundwe mkataba mpya kufikia mwaka wa 2009 utakaofanya kazi wakati mkataba wa Kyoto utakapomalizika ifikapo mwaka wa 2012. Wakati viongozi wa mataifa ya G8 watakapokutana nchini Ujerumani mwezi Juni mwaka huu, wanatakiwa wakubaliane kuhusu mkataba mpya utakaochukua nafasi ya mkataba wa Kyoto.

Mkutano wa siku mbili kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa mjini Washington uliwaleta pamoja wajumbe kutoka mataifa ya G8 na mataifa yanayoinukia kiuchumi yakiwemo Brazil, China, India, Mexico na Afrika Kusini. Mataifa ya G8 ni Uingereza, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Urusi na Marekani.

Uingereza inataka kuchukua hatua za haraka kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa. Waziri wa fedha wa Uingereza, Gordon Brown amesema mjini London kwamba inawezekana kufikia makubaliano ya kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa.

´Sio tu kwamba tunatakiwa tuchukue hatua kwa haraka kuliko hapo awali, lakini pia kuna uwezo mkubwa ukilinganisha na wakati uliopita kufikia makubaliano ya kimataifa ili kukabiliana na mabadiliko ya kimazingira.´

Naye waziri mkuu wa Uingereza, bwana Tony Blair, anaamini hata Wamarekani wameanza kubadili msimamo wao kuhusu mazingira.

´Naamini kufuatia maendeleo ya hivi karibuni tunakaribia kufikia suluhisho. Na hisia nchini Marekani nafikiri ziko katika hali ya kubadilika.´

Baada ya kumalizika mkutano wa mjini Washington viongozi walikubaliana kwamba mazungumzo yote kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na ongezeko la joto duniani yanatakiwa yamalizike ifikapo mwaka wa 2009 ili mkataba mpya uanze kufanya kazi kuanzia mwaka wa 2012.

Mjumbe wa Ujerumani katika mkutano huo, Hans Schnellhuber, aliwaambia waandishi wa habari mjini Washington baada ya mkutano kumalizika kwamba kalenda waliyojiwekea ina nia kuu, lakini haiwezekani kukosa kuitimiza. Taarifa ya pamoja ya mkutano huo isiyo na mafungamano yoyote, inataka makubaliano ya kimataifa yajumulishe kuwekwa kwa viwango vya muda mrefu vya kupunguza gesi kutoka viwandani kwa mataifa yaliyoendelea kiviwanda, mataifa yanayoendelea na hatua za kupunguza uharibifu wa misitu.

Wakati huo huo, makamu wa rais wa zamani wa Marekani, Al Gore na waandalizi wa mpango wa Live 8, wanapanga kufanya maonyesho ya muziki ya muda wa siku moja kuuhamasisha ulimwengu kuhusu hatari ya mabadiliko ya hali ya hewa. Maonyesho hayo yanayoandaliwa kufanywa tarehe saba mwezi Julai mwaka huu katika miji mikubwa duniani kote yanalenga pia kuwahimiza watu wachukue hatua za dharura kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.