Mkutano kuhusu Iran mjini Berlin
9 Mei 2007Wawakilishi wa madola makuu wanachama wakudumu wa baraza la usalama pamoja na Ujerumani,watakutana kesho mjini Berlin kuzungumzia hatua zinazobidi kuchukuliwa dhidi ya Iran pindi iking’ang’ania mpango wake wa kinuklea.
Wakurugenzi wa kisiasa wa madola manne –wanachama wakudumu wa baraza la usalama (Marekani,Urusi,Uengereza na Ufaransa,)pamoja na mwenzao wa Ujerumani watajadiliana kadhia ya Iran pembezoni mwa mkutano wa mataifa tajiri kwa viwanda G8 mjini Berlin.China,ambayo si mwanachama wa G8 inawakilishwa kwa njia ya simu katika mkutano huo wenye lengo la kujiandaa kwa mkutano uliopangwa kuitishwa wiki ijayo kati ya muakilishi mkuu wa siasa ya nje wa umoja wa Ulaya Javier Solana na mkuu wa ujumbe wa Iran katika mazungumzo ya kinuklea Ali Laridjani.
Haijulikani lakini kama mkutano huo utafanyika kama ilivyopangwa au la.
Hapo jana wawakilishi wa Iran katika mkutano wa umoja wa mataifa kuhusu mageuzi ya mkataba wa kutosambaza silaha za kinuklea mjini Vienna Austria walionyesha kuregeza kamba katika msimamo wao.Walikubali maridhiano yafikiwe kuhusu ajenda ya mazungumzo hayo na hivyo kufungua njia ya kuendelea mazungumzo yaliyokwama tangu siku kadhaa.
Suala la Iran litajadiliwa pia viongozi wa mataifa tajiri kwa viwanda G8 watakapokutana mjini Heiligandamm nchini Ujerumani,wiki chache kutoka sasa.
“Huenda wakajadiliana miongoni mwa mengineyo juu ya kuandaliwa mswaada mpya wa azimio la baraza la usalama kuhusu Iran”- amesema hayo mwanadiplomasia mmoja ambae hakutaka jina lake litajwe.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani,Sean McCormack amesema msimamo haujabadilika katika mazungumzo pamoja na Iran-lengo linasalia lile lile nalo ni kuitaka Iran iachane na mipango ya akurutubisha maadini ya Uranium.Msemaji huyo wa wizara ya mambo ya nchi za nje wa marekani ameendelea kusema tunanukuu:”mazungumzo hayawezi kuendelezwa milele kwasababu kwa namna hiyo Iran itaweza kudhibiti vizuri zaidi teknolojia mpya mpya ya kurutubisha maadini ya Uranium na kuyafanya mazungumzo yasiwe na maana tena.”
Duru za kuaminika zinasema huenda suala la kuiwekea vikwazo Iran likazingatiwa.Miongoni mwa vikwazo hivyo ni pamoja na kuzidisha orodha ya majina ya benki za Iran zilizozuwiliwa fedha zake nchi za ng’ambo.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condoleeza Rice ameshaonya,rais George W. Bush hatochelea kutumia njia za kijeshi ikilazimika ,ingawa angependelea zaidi ufumbuzi wa mzozo wa Iran kwa njia ya kidiplomasia.
Marekani na washirika wake wa Ulaya wanaituhumu Iran kutaka kutengeneza silaha za kinuklea kwa kizingizio cha kutengeneza nishati ya kinuklea.Serikali ya mjini Teheran daima imekua ikikanusha tuhuma hizo.