Mkutano kati ya viongozi wa Umoja wa Ulaya na Afrika Kusini mjini Brussels
18 Septemba 2012Huko kwenyewe Afrika Kusini wachimba migodi ya madini ya Platinum katika mashimo ya Marikana wamepunguza madai yao ya nyongeza ya mishahara, na sasa wanataka walipwe dola za Kimarekani 1,300 kwa mwezi. Hicho bado ni kima kikubwa kuliko kile kilichotolewa na waajiri wao, yaani kampuni ya Lonmin. Afrika Kusini ina uhusiano mzuri na Urusi pamoja na pia Uchina, nchi mbili ambazo zinaonekana kuwa zinakamata ufunguo katika juhudi za kuvikomesha vita vya kienyeji katika Syria. Pia katika mazungumzo baina ya pande mbili za Umoja wa Ulaya na Afrika Kusini kunazungumziwa masuala ya uchumi wa dunia na mabadiliko ya hali ya hewa duniani. Inasemekana kwamba Rais Jacob Zuma wa Afrika huenda akawaarifu maafisa wa Umoja wa Ulaya juu ya juhudi zinazochukuliwa na serikali yake za kuidhibiti migomo ya wachimba migodi katika Afrika Kusini. Katika mazungumzo hayo ya leo (18.09.2012), ujumbe wa Umoja wa Ulaya unawakilishwa na rais wa baraza la Ulaya, Herman Van Rompuy, na pia Jose Manuel Barosso, rais wa kamisheni ya Umoja wa Ulaya.
Migomo ya wachimba migodi itaathiri uchumi
Tukumbuke kwamba polisi wa Afrika Kusini waliwauwa kwa risasi wachimba migodi 34 wakati wa mapambano hapo Agosti 16, mkasa ambao ulitanda katika vichwa vya habari duniani kote. Kuna wasiwasi kwamba kisa hicho na migomo inayoendelea itaathiri uwekezaji katika uchumi wa Afrika Kusini ulio mkubwa kabisa barani Afrika. Makampuni ya kutoka nchi za Umoja wa Ulaya ndio wawekezaji wakubwa katika Afrika Kusini, yakiwekeza Euro bilioni saba mwaka 2010.
Pia nchi za Umoja wa Ulaya ndio mshirika wakubwa wa kibiashara kwa Afrika Kusini, huku asilimia 90 ya biashara yao ikiregezewa vikwazo mwaka huu, chini ya mapatano ya biashara, maendeleo na ushirikiano. Lakini Umoja wa Ulaya unaibana Afrika Kusini isonge mbele zaidi kwa kuukubali mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi wa kimkoa unaoziingiza nchi zote za jumuiya ya kiuchumi ya Kusini mwa Afrika, SADC. Kikwazo cha mwisho katika jambo hilo, kwa mujibu wa maafisa wa Umoja wa Ulaya, kinawekwa na Afrika Kusini.
Syria pia ni suala jingine muhimu linalozungumziwa kwa vile Afrika Kusini ni mwanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, tena ina maingiliano mazuri na Urusi pamoja pia na Uchina, nchi mbili ambazo zimekuwa zikizuia katika kuchukuliwa hatua dhidi ya utawala wa Syria. Masuala mengine katika ajenda ni haki za binadamu, mabadiliko ya hali ya hewa duniani, mapambano dhidi ya uharamia wa baharini na operesheni dhidi ya ugaidi katika Afrika pamoja na hali ya mambo ilivyo huko Zimbabwe.
Wakati huohuo, wachimba migodi ya madini ya Platinum wa kampuni ya Lonmin huko Marikana, kilomita 100 kaskazini magharibi ya Johannesburg, wamepunguza madai yao ya kutaka nyongeza ya mishahara, na wamesema sasa wanataka mshahara wa Rand 11,000 kila mfanya kazi, yaani dola 1,300, kila mwezi. lakini waajiri wao bado wanakiona kima hicho ni kikubwa. Kampuni hiyo ilitoa nyongeza ya baina asilimia 9 na 21, na ikasema kutoa mshahara wa Rand 12,500 kwa mwezi kutasababisha hatari ya maelfu ya wafanya kazi kupoteza ajira na kuharibu biashara ya kampuni hiyo. Bado haijulikani lini mgomo wa wafanyakazi wa migodi hiyo ya Platinum itamalizika.
Pia mwanachama muasisi wa chama tawala cha ANC katika Afrika Kusini, Julius Malema, amedai leo kwamba kuna njama ya kutaka kumuuwa ilioandaliwa na Rais Jacob Zuma. Alitoa tamko hilo baada ya polisi kumondosha kutoka mgodi wa Marikana hapo jana (17.09.2012).
Mwandishi: Othman Miraji
Mhariri: Mohammed Khelef