Mkutano kati ya Iran na Shirika la IAEA unaanza leo
26 Agosti 2005Larijani, aliyeteuliwa kushika wadhifa huo na Rais mpya wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad aliyechaguliwa mwezi wa Juni, ametoa changamoto kubwa kwa majukumu ya Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kama viongozi wa juhudi za kidiplomasia kuhusu mradi wa kinuklia wa nchi yake. Ametoa mwito kwa nchi zaidi kushiriki katika mazungumzo hayo.
Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani jana imekanusha madai hayo.
Msemaji wa Wizara hiyo, Sean McCormack amesema, “Mazungumzo yo yote yale ya kujaribu kubadilisha Wapatanishi, kusema kweli ni mbinu ya kutaka kubadilisha mada yenyewe.”
ElBaradei na Larijani, katika mazungumzo yao ya siri mjini Vienna, watazungumzia masuala yanayohusika na ukaguzi wa Shirika la Nishati ya Atomiki Ulimwenguni na hali halisi ilivyo hivi sasa.
Larijani, akinukuliwa na Televisheni ya taifa mjini Tehran ameuliza, “Kwa nini Shirika la IAEA limeruhusu mazungumzo yafanywe na nchi tatu peke yake na yategemee nchi hizo za Ulaya?” Amegusia kuwa Iran huenda ikapendekeza kuongezwa nchi nyingi zaidi katika mazungumzo hayo.
Ameongeza kusema kuwa Iran imeulizwa na nchi zisizofungamana na upande wowote ule kisiasa kwa nini mazungumzo hayo yanafanywa peke yake na nchi tatu za Umoja wa Ulaya?
Iran imezituhumu nchi hizo, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kuwa zinavuruga juhudi za kidiplomasia kwa kudai kuwa nchi hiyo lazima iache harakati zake za urutubishaji wa gesi ya kinuklia.
Shinikizo hilo linatokana na wasiwasi kuwa Iran huenda itatengeneza bomu la kinuklia ingawaje utengenezaji wa mafuta ya kinuklia unakubaliwa kwa mujibu wa mkataba wa kuzuia utengenezaji wa silaha za kinuklia (NPT).
Lakini nchi tatu za Umoja wa Ulaya zinasema kuwa Iran inapaswa kujilaumu kwa kuvunjika mazungumzo hayo kutokana na uamuzi wake mapema mwezi huu wa kurudia harakati zake za kubadilisha madini ya uranium kuwa gesi katika kiwanda chake cha Isfahan.
Hiyo ni hatua ya kwanza ya urutubishaji wa madini ya uranium ambayo ilikuwa imesimamishwa.
Kamati ya Shirika la Nishati ya Atomiki Ulimwenguni ambayo itakabidhiwa ripoti na ElBaradei kuhusu Iran Septemba 3, imeiomba nchi hiyo isimamishe tena shughuli zote.
Lakini Iran imekataa na huenda suala hili likafikishwa mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na baadaye kuwekewa vikwazo.
Ripoti hiyo ya Septemba 3 itagusia pia mradi wa Iran kuhusu madini ya plutonium ambayo nayo pia yanaweza kutengeneza bomu la atomiki.
Wakati huo huo, Wanadiplomasia wamesema kuwa Marekani na nchi tatu za Umoja wa Ulaya, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, zimekubaliana kutoitisha kikao cha dharura cha Shirika la IAEA hata ikiwa Iran itashindwa kutimiza muda wa mwisho uliowekwa na Umoja wa Mataifa wa kusimamisha shughuli zake za kutengeneza mafuta ya kinuklia. Muda wa mwisho uliowekwa ni Septemba 3, mwaka huu.
Urussi imepinga kuitishwa kwa kikao hicho kabla ya mkutano mkuu wa Viongozi utakaofanywa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Septemba 14 mpaka 16.
Wanadiplomasia wamesema kuwa Shirika la IAEA litatathmini hatua itakayochukuliwa na Iran ya utekelezaji wa azimio lake la kuitaka nchi hiyo isimamishe shughuli zake za utengenezaji wa mafuta ya kinuklia wakati wa mkutano wake wa kila robo mwaka wa Magavana wa Bodi utakaofanywa Vienna, Austria Septemba 19 baada ya mkutano mkuu wa Viongozi wa Umoja wa Mataifa.
Mkutano wa Vienna utahudhuriwa na Wajumbe kutoka nchi 35.