Mkutano juu ya usalama wa nyuklia.
13 Aprili 2010Matangazo
Rais Barack Obama wa Marekani jana aliufungua mkutano huo
kwa kuwaandalia chakula cha jioni wageni wake hao kabla ya kuanza
kikao kamili cha mazungumzo leo.
Rais Obama atawataka viongozi hao kusaini mpango wake wa
kuimarisha usalama katika ulinzi wa malighafi za kinyukilia, ambazo
haziko katika hali ya usalama, katika kipindi cha miaka minne ili
zisiweze kuangukia katika mikono ya watu wabaya.
Viongozi na maafisa waandamizi kutoka mataifa 47 duniani
wanashiriki katika mkutano huo mkubwa ulioitishwa na Rais Obama
ambao ni mkubwa kuitishwa tangu mwaka 1945, ambapo viongozi
walikutanika mjini San Francisco kwa ajili ya kuanzishwa kwa Umoja
wa Mataifa.
Ukraine nayo yaunga mkono: Saa kadhaa kabla ya kuanza kwa mkutano huo, Ukraine ilitangaza
kwamba inadhamiria kuondoa madini ya nyuklia yaliyorutubishwa
kwa hali ya juu ambayo yanaweza kutengeneza mabomu ya nyuklia
ifikapo mwaka 2012.
Akitangaza matokeo ya mkutano wa pande mbili kati ya Rais Victor
Yanukovych wa Ukraine Barack Obama, uliotoa taarifa hizo, Msemaji
wa Ikulu ya Marekani Robert Gibbs, alisema Ukraine imetangaza uamuzi muhimu kuondoa hifadhi yake yote ya
uranium iliyorutubishwa kwa kiwango cha juu hadi wakati wa mkutano
ujao wa nyuklia mwaka 2010.
Amesema hatua hiyo ni kitu ambacho Marekani imekuwa ikijaribu
kukifanya kitokee kwa zaidi ya miaka 10. na kuongeza kuwa
malighafi hiyo inatosha kutengenezea silaha kadhaa za nyuklia.
Mkutano huo wa leo utaelezea pia usalama wa wa silaha za nyuklia
pamoja na hatari ya mafuta ambayo yanatumika kwa nishati ya
matumizi ya kiraia, ambayo inaweza kutumika katika silaha na pia
mkutano huo unalenga kuzuia biashara ya magendo ya teknolojia ya
nyuklia na ujuzi wake.
Wasiwasi mkubwa ni kwa makundi ya kigaidi kama vile AlQaeda
kuweza kupata malighafi kama hizo na kutumia kufanyia
mashambulizi.
Hata hivyo baadhi ya mataifa yamekuwa na shaka kuhusiana na
uzito wa vitisho hivyo na kuangalia kama ni jinsi Marekani inavyotaka
kulishughulikia jambo hilo baada ya kukumbwa na mashambulio ya
kigaidi Septemba 11, 2001.
Lakini mshauri wa ngazi ya juu wa Rais Obama, katika masuala ya
ugaidi John Brennan ameonya kwamba Al Qaeda imekuwa
ikijaribu kupata malighafi hizo katika masoko ya wazi na katika
biashara za kihalifu.
Kwa upande wake Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ambaye
amethibitisha kuunga mkono, malengo ya Rais Obama juu ya
usalama wa nyuklia ameelezea kutokuwepo kwa mfumo wa sheria
wa kuzuia dola kutoweza kuzipajumuia za kigaidi malighafi za
kutengeneza silaha za nyuklia.
Na katika hatua nyingine, leo, Marekani na Urusi zitasaini pia
mkataba juu ya kuweka sawa hifadhi yake ya madini ya sumu kali
yanayotumika katika silaha za nyuklia.
Hata hivyo mkutano huo wa siku mbili mjini Washngton umegubikwa
na kuongezeka kwa wasiwasi juu ya Iran, ambayo Marekani na
washirika wake wanailaumu kwa kutengeneza kwa siri silaha za
nyuklia. Iran yenyewe imekuwa ikikana tuhuma hizo dhidi yake na
kusema kwamba inafanya hivyo kwa matumizi ya kiraia tu.
Katika hatua nyingine Rais Barack Obama na Rais Hu Jintao
wamekubaliana kwamba ujumbe wao utafanya kazi pamoja katika
Umoja wa Mataifa juu ya juhudi zinazoongozwa na Marekani
kuiwekea vikwazo Iran.
Mwandishi: Halima Nyanza(dpa,reuters)
Mhariri: Sekione Kitojo.
Matangazo