Mkutano juu ya usalama wa nyuklia wamalizika.
14 Aprili 2010Matangazo
Rais Barack Obama ambaye alikuwa mwenyeji wa mkutano huo
amewataka viongozi duniani kuchukua hatua ya pamoja kuzuia
makundi ya kigaidi kupata silaha za nyuklia, hatua ambayo amesema
itaifanya Marekani na dunia kwa ujumla kuwa na usalama.
Akitoa hotuba ya mwisho ya kufunga mkutano huo kuhusiana na
usalama wa nyuklia, amesema mkutano huo ni thibitisho tosha la nini
kinachowezekana, iwapo mataifa yataungana pamoja kwa ari ya
ushirikiano katika wajibu wa pamoja kukabiliana na changamoto.
Katika taarifa ya pamoja ya viongozi waliohudhuria mkutano huo,
waliunga mkono wito uliotolewa na Rais Obama wa kudhibiti vyema
malighafi za nyuklia zilizo na uwezekano wa kuathiriwa katika muda
wa miaka minne ijayo.
Katika harakati za kupambana na biashara haramu ya silaha za
nyuklia viongozi hao wamekubaliana pia kushirikiana kupeana taarifa
na upelelezi, mahakama na utaalamu mwingine wa kisheria katika
kushughulikia tatizo hilo.
Viongozi hao wamesema wametambua mahitaji ya kushirikiana
miongoni mwa mataifa kuweza kuzuia kikamilifu matukio ya biashara
haramu ya nyuklia.
Akiwa mwenyeji wa mkutano mkubwa kuwahi kufanyika nchini
Marekani kwa zaidi ya miongo sita iliyopita, Rais Obama pia
ameishinikiza China na wanachama wengine wa Baraza la Usalama
la Umoja wa Mataifa ambao wana mashaka kuunga mkono vikwazo
vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran kuhusiana na mpango wake wa
nyuklia wenye utata.
Akizungumza katika mkutano huo kuhusiana na suala hilo la Iran,
Rais Hu Jintao wa China amesema nchi yake kwa hakika inapinga
silaha za nyuklia, lakini inaunga mkono matumizi ya nyuklia kwa raia.
Kwa upande wake Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, ambaye
ameunga mkono azimio lililofikiwa katika mkutano huo, ameelezea
kufurahishwa kwake na hatua hiyo iliyofikiwa na China ya kuonesha
uwezekano wa kuchukuliwa hatua dhidi ya Iran.
Mbali na kuizungumzia Iran Rais Obama pia alielezea hofu iliyopo
kuhusiana na maghala ya silaha za nyuklia nchini Pakistan, nchi
ambayo ni ngome kubwa ya mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda na
makundi mengine ya wapiganaji.
Hata hivyo amesema nchi hiyo na
nyingine ziko katika hatua ya kukabiliana na hali hiyo ikiwemo
kutangaza hatua mpya ya kuimarisha usalama katika bandari kuzuia
biashara haramu ya nyuklia.
Naye Rais Dmitry Medvedev wa Urusi ameuelezea mkutano huo
kama wa mafanikio wakati nchi yake ikiwa imetangaza mipango ya
kufunga mtambo wake wa mwisho wa madini ya Plutonium ambayo ni
ya sumu kali yanayotumika kutengenezea silaha za nyuklia.
Afisa wa Urusi ambaye hakutaka jina lake litajwe, alilithibitishia
shirika la habari la AFP kwamba Rais Medvedev alitangaza mipango
hiyo katika mkutano wa Washington.
Mkutano mwingine wa usalama wa nyuklia unatarajiwa kufanyika
Korea ya Kusini miaka miwili ijayo.
Mwandishi: Halima Nyanza(afp,Reuters)
Mhariri: Josephat Charo
Matangazo