1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano juu ya Somalia

16 Agosti 2011

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetangaza kufanyika mkutano Septemba nne hadi sita nchini Somalia, kuandaa mpango wa kuunda serikali ya Somalia katika kipindi cha mwaka mmoja ujao.

https://p.dw.com/p/12H5Q
Misaada mbalimbali kwa ajili ya SomaliaPicha: picture-alliance/dpa

Taarifa iliyotolewa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imesema mjumbe maalumu wa umoja huo nchini Somalia Augustine Mahiga anaandaa mkutano huo.

Taarifa hiyo imesema kuwa lengo la mkutano huo ni kukubaliana juu ya mikakati muhimu na vipaumbele kwa Somalia katika kipindi cha zaidi ya miezi 12 ijayo,pakiwepo ratiba maalum na muongozo wa kufuatwa na serikali ya mpito ya Somalia inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Umoja wa mataifa umesisitiza pia kuhusu kushirikishwa makundi ya Wasomali katika mkutano huo, ikiwa ni pamoja na taasisi za serikali ya mpito, serikali za mitaa na majimbo na wadau wengine wa kisomali.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limedokeza kwamba uungaji mkono hapo baadaye kwa serikali ya mpito utakuwa kwa misingi ya ukamilishaji wa majukumu katika mpango huo.

Wakati huohuo Umoja wa Mataifa unachunguza madai ya kuibiwa chakula cha misaada kilichosafirishwa nchini Somalia kwa ajili ya kukabiliana na njaa, iliyoua maelfu ya watu.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq amesema Shirika la Umoja wa mataifa la Mpango wa Chakula litaisimamisha taasisi yoyote ile ambayo itahusika na wizi huo, kufanya kazi na shirika hilo.

Hata hivyo Umoja wa Mataifa bado haujasema ni kiasi gani cha chakula kilichoibiwa.

Amesema shirika hilo linasimamia na kudhibiti vikali nchini humo, lakini kutokana na hatari za kiusalama na vikwazo huduma hizo za usambazaji misaada ya kibinadamu kumekuwa na udhaifu mkubwa wa kuweza kuporwa, kushambuliwa na hila za makundi ya wapiganaji.

Tangazo la uchunguzi huo limekuja katika siku ambayo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa wito kwa serikali kukubali ombi lililotolewa na umoja huo la kutoa dola bilioni 2.4 kupambana na ukame mashariki ya Afrika.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloratibu misaada ya dharura, zaidi ya watu milioni 12.4 wako katika hatari ya kukumbwa na njaa.

Katika taarifa yake serikali ya mpito ya Somalia imesema ina sera makini katika kukabiliana na rushwa na uhalifu dhidi ya chakula cha msaada.

Aidha imesema taarifa hizo za kuibiwa kwa chakula zisitumiwe kama sababu kudhorotesha usambazaji wa msaada kutokana na hali hiyo kuweza kusababisha vifo zaidi vya watu kutokana na baa la njaa.

Tayari kikosi maalumu kimeundwa kuweza kulinda chakula na usambazaji wake katika makambi.

Mashirika ya Umoja wa mataifa yamekuwa yakihangaika kuweza kupeleka misaada ya chakula katika maeneo ya Somalia ambayo yanadhibitiwa na wapiganaji wa al Shabaab.

Mwandishi: Halima Nyanza(dpa,afp)

Mhariri: Hamidou Oummilkheir