1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkurugenzi mteule wa WHO Afrika Ndugulile afariki India

27 Novemba 2024

Mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani - WHO kanda ya Afrika Dr. Faustine Ndugulile, amefariki dunia alipokuwa akitibiwa nchini India.

https://p.dw.com/p/4nTmm
Republik Kongo Brazzaville | Dr. Faustine Engelbert Ndugulile
Dokta Faustine Engelbert Ndugulile wa katikati akiwa na maafisa wengine waandamizi wa WHO.Picha: WHO/Daniel Elombat

Hayo yametangazwa na Spika wa bunge la Tanzania Tulia Ackson. Kabla ya kifo chake, Ndugulile alihudumu kama mbunge wa Kigamboni katika jiji la kibiashara la Tanzania, Dar es Salaam. Pia alikuwa waziri msaidizi wa afya kati ya mwaka wa 2017 na 2020 na waziri wa habari na mawasiliano hadi mwaka wa 2021. Alichaguliwa kuwa mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika Agosti mwaka huu na alitarajiwa kuanza majukumu yake Februari mwakani, akimrithi Dr. Matshidiso Moeti aliyehudumu katika wadhifa huo kwa mihula miwili. Katika hotuba yake ya kuukubali wadhifa huo, Ndugulile alielezea dhamira thabiti ya kuendeleza sekta ya afya na ustawi wa watu barani Afrika. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi akielezea kifo chake kuwa msiba mkubwa, naye Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Ghebreyesus akisema ameshtushwa na kuhuzunishwa na kifo chake. Spika Tulia Ackson amesema mipango ya kuurejesha mwili wake nyumbani inaendelea, akiongeza kuwa mipango ya mazishi itatangazwa baadae.