1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Vladimir Kara-Murza ahukumiwa kifungo cha miaka 25 jela

17 Aprili 2023

Mkosoaji wa ikulu ya Urusi, Kremlin, Vladimir Kara-Murza amehukumiwa kifungo cha miaka 25 jela na mahakama moja ya Moscow, hii ikiwa hukumu kali zaidi ya aina yake tangu Urusi ilipoivamia Ukraine

https://p.dw.com/p/4QCbl
Putins jährliche Ansprache vor der Bundesversammlung in Moskau
Picha: Sergei Karpukhin/TASS/IMAGO

Kara-Murza, mwenye umri wa miaka 41, baba ya watoto watatu na mwanasiasa wa upinzani mwenye uraia wa Urusi na Uingereza, ametumia miaka mingi kumshtumu Rais Vladimir Putin na kuyashinikiza mataifa ya Magharibi kuiwekea vikwazo Urusi na watu binafsi wa taifa hilo kwa madai ya ukiukaji wa haki za binadamu. Waendesha mashtaka waliokuwa wameiomba mahakama kutoa hukumu hiyo ya kifungo cha miaka 25 jela, walikuwa wamemshtumu kwa uhaini na kulidharau jeshi la Urusi baada ya kukosoa kile ambacho Urusi ilikitaja kuwa operesheni maalumu ya kijeshi nchini Ukraine.

Wakili wa Kara- Murza akosoa hukumu hiyo

Akizungumzia hukumu hiyo, wakili wa Kara-Murza Maria Eismont amesema kuwa kifungo cha miaka 25 katika jela lenye ulinzi mkali,  ndio hukumu ya juu kwa mtu ambaye hajawahi kushtakiwa tena. Eismont ameongeza kuwa, hakuna uwezekano kwamba Vladimir, ambaye ni baba wa watoto watatu, anaweza kuhukumiwa kwa kiwango hiki cha juu, ikiwa sheria itafuatwa.

Umoja wa Mataifa washutumu hukumu dhidi ya Kara- Murza

Josep Borrell
Josep Borrell - Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Picha: DW

Umoja wa Mataifa pia umeshtumu hukumu hiyo ya Kara-Murza na kuielezea kuwa kali na iliyochochewa kisiasa. Katika taarifa, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell, amesema kuwa uamuzi huo wa mahakama unaashiria kwa mara nyingine tena matumizi mabaya ya idara ya mahakama ili kuwashinikiza wanaharakati, watetezi wa haki za binadamu na sauti zozote zinazopinga uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Borrell ameongeza kuwa wanatoa wito kwa Urusi kuwaachia huru kwa haraka na bila masharti wale wote waliofungwa kwa mashtaka yaliochochewa kisiasa.

Mpango wa nafaka wa Bahari Nyeusi wakabiliwa na hatari ya kukatizwa

Wakati huo huo, wizara inayohusika na ujenzi mpya wa nchi nchini Ukraine, imesema mpango wa nafaka wa Bahari Nyeusi unakabiliwa na hatari ya kukatizwa baada ya Urusi kwa mara nyingine tena kuzuia ukaguzi wa meli katika bahari ya Uturuki. Mpango huo unawezesha usafirishaji salama wa nafaka kutoka baadhi ya bandari za bahari nyeusi za Ukraine kufuatia uvamizi wa Urusi nchini humo. Katika ujumbe kupitia mtandao wa Facebook, wizara hiyo inayohusika na ujenzi mpya wa nchi imesema kuwa kwa mara ya pili katika muda wa miezi tisa ya kuendelezwa kwa mpango huo wa nafaka, hakuna mpango wa ukaguzi uliowekwa na hakuna meli hata moja iliyokaguliwa na kwamba hii inatishia utendaji kazi wa mpango huo wa nafaka.