Mke wa rais Mugabe arejea nyumbani Zimbabwe
16 Agosti 2017raceGHapakuwepo na taarifa zozote kumuhusu Bi Grace Mugabe, mwenye umri wa miaka 52, lakini duru za serikali ya Zimbabwe zimetoa taarifa kuwa mke huyo wa rais wa Zimbabwe alikuwa tayari ameshawasili nyumbani. Vyanzo hivyo hivyo vya serikali ya Zimbabwe vilionyesha kushangaa kwao na taarifa za tuhuma zinazomkabili Bi Grace Mugabe.
Taarifa kutoka polisi ya nchini Afrika Kusini zinasema Grace Mugabe hakufika katika kituo cha polisi, licha ya kukubali kuwa angeenda. Tuhuma zinazomkabili mwanamke huyo anayetazamwa na wengi kama mrithi mtarajiwa wa mumewe mwenye umri wa miaka 93, zimezusha sintofahamu kwani mapema jana waziri anayehusika na maswala ya polisi nchini Afrika Kusini, Fikile Mbalula, alisema kuwa Bi Grace Mugabe alikuwa tayari ameshajisalimisha kwa polisi na kwamba angefikishwa mahakamani katika muda usiokuwa mrefu. Hata hivyo, hali halisi haikuwa hivyo kwani hadi muda wa kufunga kazi unafika, Bi Grace Mugabe alikuwa hajafikishwa mahakamani hapo.
Mrembo Gabriella Engels aliwaambia waandishi wa habari wa Afrika Kusini kwamba Grace Mugabe alimshambulia baada ya yeye kwenda kuwatembelea wana wawili wa Rais Mugabe, Robert na Chatunga, katika hoteli moja ya kifahari iliyo katika wilaya ya Sandton mjini Johannesburg.
Mwanamitindo huyo amefahamisha kwamba Bi Grace Mugabe aliingia chumbani akiwa ameshikilia waya na hapo akaanza kumchapa na kumsababishia jeraha kwenye uso wake, kitendo ambacho kwanza kilimshangaza na kumfanya achangayinikiwe kwani hakuwa amemjua mama huyo kuwa ndiye mke wa Rais Mugabe na mama wa wavulana wale. Mrembo huyo amesema alilazimika kutambaa hadi nje ya chumba kabla ya kupata nafasi ya kukimbia. Engels amesisitiza kuwa anataka haki itendeke.
Taarifa zaidi zinaarifu kwamba watoto hao wa Rais Mugabe walishawahi kufukuzwa kutoka kwenye hoteli hiyo ya kifahari siku za nyuma kutokana na rabsha zilizotokea usiku wa manane. Meneja wa hoteli hiyo amewaambia waandishi wa habari kwamba watoto hao wa Rais Mugabe hawako hotelini hapo kwa sasa.
Hata hivyo, waziri anayehusika na maswala ya polisi nchini Afrika Kusini, Fikile Mbalula, amesema watamshtaki Bi Grace Mugabe japokuwa ana kinga ya kidiplomasia.
Mwandishi: Zainab Aziz/AFPE/RTRE
Mhariri: Mohammed Khelef