Mkataba wa wakimbizi watimiza mwaka mmoja, hali bado mbaya
17 Desemba 2019Wakimbizi wenye fadhaa nchini Uganda wanatumia kila njia waijuwayo kuweza kuishi kutokana na huduma dhaifu wanazopata makambini, kwani michango ya mashirika ya kibinaadamu imepunguwa sana.
Watu wanaingia kwenye madeni, wanalazimika hata kukosa baadhi ya milo ili kuhifadhi chakula, wazazi wanawauwa watoto wao wa kike na waomba hifadhi wanajihusisha na vitendo vya ngono ili tu wajikimu kimaisha.
Mkurugenzi Mkaazi wa Baraza la Wakimbizi la Norway nchini Uganda, Ulrika Blom, anasema taifa hilo la Afrika Mashariki liko kwenye ukingo wa kuporomoka panapohusika suala la wakimbizi.
"Linapambana kukimu mahitaji ya kibinaadamu ya wakimbizi ambao nao wanazidi kuongezeka, ambao nao wanakabiliwa na madeni na hatari kwa sababu hakuna fedha za kuwasaidia," alisema Blom kwenye taarifa yake kwa waandishi wa habari.
Kwa sasa, Uganda inawahifadhi wakimbizi zaidi ya milioni 1.3, ikiwa ni ya tatu duniani kwa kuwa na wakimbizi wengi baada ya Uturuki na Pakistan.
Licha ya watu wengi zaidi kuingia nchini humo, kiwango cha fedha za kuwahudumia mwaka 2019 kilisalia kuwa cha chini sana. Hadi mwezi wa Disemba, ni asimilia 39 ya fedha zilizokuwa zimepatikana.
Wakimbizi wa Venezuela hali mbaya
Nchini Venezuela, kila siku mamia ya raia wanaanza safari ya mateso kuelekea kule wanakodhani kuna maisha mazuri zaidi. Inawachukuwa siku tano nzima kutoka mji wa mpakani na Colombo uitwao Cucuta hadi mji mkuu, Bogota, huku kiwango cha bahari kikipanda kutoka mita 320 hadi 2,640. Na kila siku watu wanakufa. Watoto hasa ndio wanaopoteza maisha kutokana na machofu, baridi kali au matatizo ya kupumua.
Tangu Rais Nicolas Maduro ashinde vita vyake vya kuwania madaraka dhidi ya rais aliyejitangaza mwenyewe, Juan Guaido, mwanzoni mwa mwaka huu, dunia hailezwi mengi juu ya majaaliwa ya wakimbizi wa Venezuela.
Lakini hiyo haimaanishi kuwa idadi yao imepunguwa. Tangu mzozo huo uanze, watu milioni nne na laki nane wameshaikimbia nchi hiyo ya Amerika Kusini, huku milioni 3.9 wakiishia kwenye eneo hilo hilo, hasa nchi jirani, Colombia.
Msemaji wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, Olga Sarrado, anasema kuwa Colombia nayo huenda karibuni ikazidiwa, maana mataifa mengine jirani ya Ecuador, Peru na Chile yameweka vikwazo kadhaa kuwapatia ruhusa ya kuingia wakimbizi wa Venezuela.
Mifano hii miwili ya Uganda iliyo mashariki mwa Afrika na Colombia iliyo Amerika Kusini, inasema kitu kimoja tu: nacho ni kuwa licha ya Mkataba wa Kilimwengu wa Kuwalinda Wakimbizi, mwaka huu mmoja umepita ukiwa haujashuhudia mabadiliko yoyote kwenye hali za wakimbizi ulimwenguni.