Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Uhamiaji ni upi?
2 Novemba 2018Mkataba wa Umoja wa wa Mataifa kuhusu uhamiaji salama, wenye utaratibu na wa kawaida, unaashiria mwanzo wa taasisi hiyo ya kimataifa kukubaliana na mikakati ya kimataifa ya kukabili athari na changamoto zinazohusiana na uhamiaji, na wakati huo huo kuongeza manufaa kwa nchi ambazo zinawapa hifadhi wahamiaji.
Mkataba huo unakuja katika wakati ambapo idadi kubwa ya watu duniani, ambao mara nyingi wanakimbia kutokana na vita na umaskini, wanazikimbia nchi zao kutafuta hifadhi kwingine. Hata hivyo si nchi zote zinazokubaliana na mkataba huo, na zimekuwa zikipaza sauti kuhusu sababu za kuukataa.
Kuandikwa kwake kulikamilishwa na mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa mnamo tarehe 13 Julai mwaka huu wa 2018, na umeratibiwa kupitishwa mwezi Desemba wakati wa mkutano wa serikali mbalimbali utakaofanyika mjini Marrakesh, Morocco. Mkataba huo umejikita katika kutambua haja ya dunia nzima kushirikiana iwapo uhamiaji unaoendelea sasa na utakaoendelea siku za baadaye utahitaji kudhibitiwa kwa njia za ubinadamu huku pia ikizingatiwa umuhimu wa kuwepo uhuru wa nchi. Kadhalika unajumuisha malengo 23 ya usimamizi wa msuala ya uhamiaji katika ngazi za nchi husika,kitaifa,kikanda na hata kimataifa.
Hata hivyo haijataja idadi ya wahamiaji ambayo nchi inafaa kukubali. Mkataba huo pia unataka ulanguzi wa watu ukabiliwe, na usimamizi jumuishi na salama wa mipaka. Kulinagana na Umoja wa Mataifa makubaliano hayo kwa pamoja yanaangazia wasiwasi uliopo wa mataifa na jamii, na suala kwamba matokeo ya uhamiaji kwa kila nchi husika na maeneo yanaweza kutofautiana kulingana na idadi ya watu, uchumi, na hali ya mazingira.
Licha ya kuwapo kwa hakikisho hilo, na suala kwamba mkataba huo haufungamanishi kisheria, haijakuwa rahisi kuwashurutisha baadhi ya wanachama wa Umoja wa Mataifa, wakiwemo Marekani, Austria na Hungary ambazo zimeshasema hazitousaini mkataba huo. Serikali za nchi hizo zimetoa pingamizi, miongoni mwa masuala mengine yakisema kuwa mkataba huo unachanganya haki ya wanaotafuta hifadhi na za wahamiaji wa kiuchumi.
Marekani chini ya uongozi wa Rais Donald Trump pia inasema mikataba ya kimataifa, hasa mkataba huu, inakwenda kinyume na uhuru wa utawala wa serikali za nchi wanachama. Katika juhudi za kukabiliana na taarifa potofu zinazosambazwa mitandaoni kuhusu mkataba huo wa Umoja wa Mataifa kuhusu Uhamiaji Duniani,chama cha Kansela wa Ujerumani Angela Merkel CDU, kimechapisha orodha ya maswali na majibu ili kuwahakikishia raia wenye hofu. Vile vile hatua hiyo imeonekana kupuuza pingamizi zilizotolewa na mataifa yanayokata kutia saini mkataba huo.
CDU pia inasisitiza kwamba mkataba huo unataka kuimarisha ulinzi wa mipaka ya kitaifa na si kuidhoofisha. Kadhalika CDU imesema mkataba huo umejumuisha masuala ya uhuru wa uongozi katika masuala yote ya mipaka na usalama kuhusu uhamiaji, na imefafanua wazi wazi kati ya uhamiaji halali na usiokubalika.
Mwandishi: Sophia Chinyezi/DW
Mhariri: Saumu Yusuf