1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkataba wa START huenda ukaidhinishwa leo na baraza la Seneti

Sekione Kitojo22 Desemba 2010

Rais Dmitry Medvedev wa Urusi amesema kuwa anamatumaini baraza la Seneti la Marekani litauidhinisha mkataba wa START

https://p.dw.com/p/zoS1
Rais wa Urusi Dmitry Medvedev.Picha: AP

Rais Dmitry Medvedev wa Urusi amesema leo kuwa anamatumaini kuwa baraza la seneti la Marekani litaidhinisha mkataba wa upunguzaji wa silaha za kinuklia wa START ambao ni muhimu kwa kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili.Kura ya kuidhinisha mkataba huo hata hivyo itafanyika leo Jumatano.

Medvedev amesema kuwa iwapo Urusi itashindwa kujiunga na mfumo wa ulinzi dhidi ya makombora pamoja na NATO, Marekani pamoja na Urusi zitajikuta zikifanya maamuzi magumu yasiyopendeza, na kusisitiza madai ya serikali ya Urusi ya kuwa jukumu muhimu katika mpango huo wa Ulaya wa ulinzi wa makombora. Medvedev alikuwa akizungumza wakati wa ziara nchini India kabla ya baraza la Seneti kupiga kura ya kuidhinisha mkataba huo.

Upinzani wa wabunge wa chama cha Republican dhidi ya mkataba huo wa START, uliporomoka kutokana na kwamba kuidhinisha mkataba huo wa kupunguza silaha kulikuwa na mbinyo mkali. Mawaziri wote wa kutoka chama cha Republican ambao waliwahi kuwa katika wadhifa wa waziri wa mambo ya kigeni, waziri wa ulinzi Robert Gates na mwenyekiti wa jopo la wanadhimu wakuu wa jeshi Mike Mullen kwa pamoja wamesema kuwa mkataba huo ni lazima uidhinishwe kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Katika mkutano wa jumuiya ya NATO mjini Lisbon mataifa kadha ya Ulaya kuanzia Lithuania na Norway, kutoka Denmark hadi Hangary na Bulgaria wamekubali wazo la kuwa na mkataba kama huo. Hata kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameeleza kuwa anamatumaini kuwa mktaba wa START utaidhinishwa.

Rais Obama Jumamosi iliyopita alitumia hotuba yake ya kila wiki kwa njia ya radio kuzungumzia kuhusu mkataba huo wa START, na kusisitiza juu ya umuhimu wake.

Obama Afghanistan USA Pakistan
Rais Barack ObamaPicha: AP

"Bila ya kuwa na mkataba kama huu tunahatarisha kurejesha nyuma hatua zilizopigwa katika ushirikiano wetu na Urusi. Ushirikiano ambao ni muhimu katika kutekeleza vikwazo imara dhidi ya Iran, kulinda maada muhimu za kinuklia dhidi ya magaidi, na kupeleka misaada muhimu kwa vikosi vyetu nchini Afghanistan".

Maseneta wa chama cha Republican hawakutaka kuzuwia uamuzi huo kama walivyofanya katika baraza la zamani, wakati huu ambapo kwa kura za wabunge wa chama hicho kutapatikana wingi wa kuidhinisha mkataba huo. Baraza la Seneti linapaswa kuupitisha mkataba huo kwa wingi wa theluthi mbili, ikiwa ni kura 67 , iwapo maseneta wote 100 watakuwapo katika upigaji kura. Kuanzia Januari kura 14 za Warepublican zitakuwa ni muhimu, kwa sababu katika uchaguzi wa baraza la Congress mwezi Novemba mwaka huu Warepublican walipata viti zaidi katika baraza la seneti.

Mkataba wa START ulitiwa saini tarehe 8 Aprili mwaka huu na rais Barack Obama pamoja na mwenzake wa Urusi Dimitry Medvedev. Mkataba huo unataka kupunguzwa kwa makombora ya kinuklia kufikia kiwango cha 1550 katika pande zote mbili. Idadi ya mifumo ya kufyatulia makombora hayo , nyambizi pamoja na ndege za kivita vinapunguzwa kwa kila nchi na kufikia 800 tu.

Mwandishi : Bergmann, Christina / ZR / Sekione Kitojo

Mhariri: Abdul-Rahman