Mkataba wa nuklea wa Iran na kutojua kusoma Magazetini
8 Mei 2019Tunaanza na makubaliano ya kimataifa kuhusu mradi wa nyuklia wa Iran ambayo leo hii umekamilika mwaka mmoja tangu rais wa Marekani Donald Trump alipoamua kuyavunja. Serikali ya Iran inashurutisha kuendelea kuheshimu makubaliano hayo na masharti kadhaa. Gazeti la Rheinpfalz linaandika kuhusu makubaliano ya mradi wa nuklea wa Iran:
"Kwamba vikwazo vinaiumiza vibaya sana Iran, hilo hakuna anaelibisha. Sarafu ya Iran, Rial inapoteza thamani. Ughali wa maisha umefikia asili mia 40.
Mafuriko mabaya kabisa yalipolikumba eneo la Uajemi mwezi Machi na Aprili iliyopita, wakimbizi wa Iran wanaoishi ughaibuni walishindwa kuwasaidia jamaa zao nyumbani kwa sababu ya vikwazo vya Marekani vinavyotishia kuzichukulia hatua kali benki zote zitakazofanya biashara na Iran. Ikiwa katika hali kama hiyo mkuu wa vikosi vya wanajeshi vya Iran Mohammed Baqeri anatishia kuifunga njia ya kuingia katika Ghuba la Uajemi, hali hiyo inabainisha jinsi Iran inavyohisi inakabwa. Na pindi ujia wa maji wa Hormuz ukifungwa-basi moja kwa tano ya meli zinazosafirisha mafuta duniani zitakwama.
Uchaguzi wa meya wa istanbul warudiwa Uturuki
Nchini Uturuki, tume ya uchaguzi imeamua urudiwe tena uchaguzi wa meya wa jiji la Istanbul . Uamuzi huo umepitishwa licha ya kwamba matokeo yalitangazwa na mshindi kukabidhiwa wadhifa wake. Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanashuku kama rais Recep Tayyip Erdogan na chama chake cha kihafiidhina cha itikadi kali na ambae binafsi ameanza kupanda daraja ya kisiasa kutoka Istanbul hakushawishi uamuzi huo. Gazeti la Fuldaer Zeitung linaandika:
"Baada ya kuendesha wadhifa wake kwa muda wa wiki tatu, mshindi wa uchaguzi katika jiji la Istanbul, Ekrem Imamoglu wa chama cha CHP ametambua kwa mara nyengine tena katika ujia wa maji wa Bosporus, unaoigawa Ulaya na Asia, Demokrasia sio kipa umbele, kinachopewa umuhimu mkubwa zaidi ni ridhaa ya rais mwenye madaraka makubwa kupita kiasi. Na mkono wa Recep Tayyip Erdogan unafika mbali. Kwa hivyo kulitaja zoezi la uchaguzi kuwa ni "ushindi wa demokrasia" ni dharau ya mtawala wa kiimla anaetumia neno demokrasia na muongozo wa nchi inayofuata sheria kama pazia la kisiasa."
Wasojua kusoma na kuandika Ujerumani
Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu idadi ya wasiojua kusoma na kuandika nchini Ujerumani. Gazeti la "Neue Osnabrücker Zeitung" linaandika: "Idadi yenyewe kwanza inashangaza na inaonyesha kuwa ni ya aibu katika nchi kama hii ya watunzi na wasomi. Watu milioni sita na laki mbili, kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa hivi karibuni, wana shida za kusoma na kuandika. Lakini unapotupia jicho takwimu hizo hutakosa kugundua ,ingawa kuna kivuli lakini pia mwangaza upo.
Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/INlandspresse
Mhariri: Gakuba, Daniel