1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkasa wa Zidane na Materazzi mbele ya mahkama ya FIFA

Ramadhan Ali14 Julai 2006

Al Ahly mabingwa wa Afrika warudi uwanjani mwishoni mwa wiki kutetea taji lao.Zidane na Materazzi kujieleza mbele ya Tume ya nidhamu ya FIFA na kocha mpya wa ujerumani-Joachim Löw kuendeleza alipoacha Klinsmann.

https://p.dw.com/p/CHdX
Finali ya Kombe la dunia-Itali na Ufaransa kuchezwa tena ?
Finali ya Kombe la dunia-Itali na Ufaransa kuchezwa tena ?Picha: AP

Jumamosi hii tunawachukua katika changamoto za Kombe la klabu bingwa barani Afrika; mkasa wa Zinedine Zidane na Marco Materazzi kuchunguzwa na FIFA na je, finali ya Julai 9 ya kombe la dunia yaweza kurudiwa kama anavyodai wakili wa Zidane ?

Kashfa ya vilabu vya Itali –je, klabu ziadhibiwe kwa kuteremshwa daraja au viongozi wa vilabu ndio waadhibiwe kama anavyodai waziri mkuu wa zamani Berlusconi-anaemiliki timu ya AC Milan.Nani kocha mpya wa Ujerumani Joachim Löw aleichukua wadhifa wa Jürgen Klinsmann ?

Jioni hii,mabingwa wa Afrika Al Ahly ya Misri wamerudi uwanjani kutetea taji lao walilolitwaa mwaka jana walipoitimua nje Etoile du sahel ya Tunisia.Jumamosi hii wana miadi na timu nyengine ya Tunisia-CS Sfaxien.Al Ahly inalenga kusawazisha rekodi yake na Zamalek ya Misri kuvaa taji hili mara 5.Isitoshe, Al Ahly inatetea rekodi nyengine-ile ya kutofungwa kwa kipindi cha miaka 2 tangu nyumbani hata barani Afrika.

Mara ya mwisho Al Ahly kulazwa ilikua pale ilipochapwa mabao 2-1 na Arab Contractors ya Misri, Julai 2,2004.

Kabla kuingia uwanjani leo, Al Ahly ilijiandaa nchini Ufaransa na ilitoka sare bao 1:1 na Paris St.Germain jumaane iliopita.Kwa bahati mbaya, al Ahly haichezi leo na mshambulizi wao hatari Mohamed Barakat pamoja pia na beki wa taifa Mohamed Abdelwahab ambae yumo matatani kimkataba.

Kesho kuna mapambano zaidi:JS Kabylie ya Algeria ina miadi na Asante kotoko ya Ghana.Katika kundi B, mabingwa mara 2 wa Afrika-Enyimba ya Nigeria wanakutana kesho na Hearts of Oak ya Ghana wakati Orlando Pirates ya Afrika Kusini wanawakaribisha mjini Johannesberg, Asec Abidjan ya ivory Coast hapo jumaane.Pirates waliruhusiwa kuahirisha mpambano wao huu kwavile wanacheza leo mechi ya kirafiki na Manchester United ya Uingereza mjini Durban.

Tukisalia katika medani ya dimba barani Afrika,

timu kadhaa za taifa za afrika wiki hii zilitangaza makocha wapya na kuwauzulu wale wa zamani:

Tanzania, Kongo-Brazzaville,Uganda,Botswana zote zimejipatia kocha mpya.Mpya kutangaza jana ni Burkina Faso ambayo imemuajiri upya Idrissa Traore anaechukua nafasi ya Bernard Simondi alietimuliwa wiki iliopita.

Kocha Traore pia aliongoza B.Faso kutoka 1993 hadi 1996.Alitimuliwa lakini pale B.Faso ilipokomewa mabao 5-1 na Zambia katika duru ya kwanza ya finali za Kombe la Afrika la Mataifa 1996 nchini Afrika kusini.

Anatarajiwa kuiandaa B.Faso kwa changamoto za kuania tiketi za finali ya Kombe la Afrika ,2008 nchini Ghana:

Chamngamoto hizo zinaanza Septemba na Burkina Faso imeangukia kundi la 7 linalojumuisha Tanzania,Msumbiji na Senegal.

Mpambano wa kwanza wa kocha Traore utakua na Morocco mjini Rabat hapo August,16.

Nje ya dimba la Afrika, FIFA-shirikisho la dimba ulimwenguni-limeanza uchunguzi upande wa beki wa Itali-mabingwa wa dunia-Marco Materazzi kujua alimtukana nahodha wa Ufaransa Zinedine Zidane kwa maneno gani ?

Zidane alitimuliwa nje ya uwanja na rifu pale mpambano wao uliporefushwa na kufuatia Zidane kumpiga Materazzi dafurao.Zidane alitaka radhi kwa madhambi hayo aliofanya m bele ya hadhara nzima ulimwenguni ,lakini alisema hajuti kwanini alimtandika kichwa Materazzi.

Kama sehemu ya uchunguzi huu unaoendelea, Zidane atapewa nafasi ya kujieleza kimaandishi hadi Julai 18 mambo yalianza vipi na kumalizikia vipi .Baadae Materazzi atatakiwa ajibu pia kimaandishi tuhuma za Zidane.Wachezaji wote 2 wameitwa kukabiliana uso kwa uso mbele ya kikao cha kamati ya nidhamu ya FIFA hapo Julai 20 mjini Zurich.

Zidane alikwishatangaza kwamba anastaafu katika dimba baada ya kombe la dunia,lakini baada ya mkasa uliotokea anajiokuta bado anacheza dimba ingawa nje ya chaki ya uwanja.Zidane ndie alieipatia Ufaransa bao lake la kwamnza alipopiga mkwaju wa penalty maridadi ajabu.

Materazzi akajibisha kwa bao la kichwa alipoifumania kona katika lango la Ufaransa.

Wakili wa Zidane,mfaransa Mehana Mouhou anapanga kuitaka mahkama kujiingiza katika kisa hiki na hasa kule kutolewa nje ya uwanja kwa Zidane na rifu.Anatia shaka shaka iwapo rifu 4 uwanjani alitegemea mchezo ulivyokwenda na sio video kuamua hatima ya Zidane .

Ikiwa itabainika kwamba rifu huyo 4 alitumia ushahidi wa video uwanjani ,basi FIFA itabidi kuamua finali ya jumapili iliopita irudiwe-asema wakili huyo.

Sheria za FIFA zinakataza marifu kutumia ushahidi wa video wakati wa mechi kuamua.

Itali sio tu bado imekumbwa na kisa cha Materazzi na Zidane, bali baada ya kujiuzulu kwa kocha wake Marcello Lippi na kumuajiri kocha mpya Roberto Donadoni,Itali inasubiri hukumu juu ya hatima ya klabu zake mashuhuri.Klabu 4 maarufu za Itali na wakuu 25 wa klabu hizo wakingoja kwa hamu kuu kusikia hukumu juu ya hatima yao.

Mabingwa Juventus ,klabu ya waziri mkuu wa zamani Berlusconi-AC Milan, Fiorentina na Lazio Roma pamoja na wakubwa 25 tangu wa vilabu hivyo hata wa shirikisho la mpira la Itali,marifu na washika bendera wameshtakiwa kupangilia matokeo ya mecgi za Ligi ya Itali msimu wa 2004/5.

Juventus lakini ndio shina la kashfa hii. Ikitazamiwa adhabu ni kuziteremsha tu timu hizo daraja ya tatu.Wote wenye hatia wana haki ya kukata rufaa.Waziri mkuu wa zamani Silvio Berlusconi,alipendekeza kati ya wiki hii kabla kutoka hukumu hiyo kuwa wakubwa wa vilabu ndio waadhibiwe na sio klabu zenyewe.

Berlusconi ndie mwenye kuimiliki klabu ya AC Milan.

Wakati Itali imejipatia kocha mpya roberto Donadoni, Ujerumani pia imepata kocha mpya –aliekua msaidizi wa Klinsmann.Nae ni Joachim Löw ambae Klinsmann amedai hakuwa msaidizi bali mshirika wake.

Nani Joachm Löw ?

Löw mwenye umri wa miaka 46,hakua mchezaji dimba maarufu kama Klinsmann,bali mchezaji wa wastani aliecheza misimu 2 tu katika Bundesliga.Alizichezea timu za Eintracht Frankfurt na Karlsruhe.Alipitisha muda mwingi akiichezea Freiburg katika daraja la pili kabla kuwa kocha.

Lakini, aliposomea ukocha wa dimba alikua darasa moja na Klinsmann aliezichezea hapo kabla timu kama Stuttgart,Bayern munich,Inter Milan,Monaco na Tottenham Hotspurs.

Wote wawili-Löw na Klinsmann wanakubaliana juu ya falsafa moja ya mchezo na jinsi ya kuwatia shime wachezaji kucheza nguvu-moja na kwa ari moja.

Löw alianza kuwa kocha wa timu ya chipukizi ya Winterthur nchini Uswisi kabla kushika usukani wa kuiongoza stuttgart 1996 na kuipatia nafasi ya 4 katika ngazi ya Bundesliga na mwishoe kuitawaza mabingwa kombe la Ujerumani 1997.

Baadae akawa kocha wa Fernerbahce ya uturuki na baadae akahamia Austria ambako alinyakua taji la ubingwa na FC Tirol msimu wa 2001-2002.

Löw alianza kujenga jina la kocha wa kuaminika ,lakini kama Klinsmann akiwaumiza vichwa viongozi wa klabu alizozifunza.

Alipoteuliwa Klinsmann kocha wa Ujerumani, alihitaji mtu mwenye sifa kama hizo na jina la Joachim Löw mara alilikumbuka.

Löw alifika hadi kushambuliwa kuwa hana maarifa ya kutosha ya ukocha kufunza klabu mashuhuri seuze timu ya taifa.

Aleimkosoa si mwengine, bali Uli Hoeness-meneja wa Bayern Munich.Jürgen Klinsmann lakini,alimtetea mshirika wake na shirikisho la dimba la Ujerumani, likamuidhinisha kuwa msaidizi wa kocha Klinsmann.

Kuanzia wiki hii, Joachim Löw ndie kocha kamili wa timu ya Taifa na ndie atakaeiongoza Ujerumani kukata tiketi yake kwa Kombe lijalo la Ulaya la Mataifa nchini Uswisi,2008.