Mkasa wa vimbunga Kentucky watangazwa kuwa janga la nchi
13 Desemba 2021Katika taarifa kutoka ikulu ya White House, rais Biden ameutaja mkasa huo kuwa moja kati ya mikasa mibaya zaidi ya vimbunga kutokea katika historia ya Marekani huku maafisa wa serikali na eneo hilo wakitahadharisha kuwa idadi ya vifo ambayo kwasasa imefikia watu 94 huenda ikaongezeka zaidi. Rais Biden, amewatuma viongozi wa wizara ya usalama wa kitaifa na idara ya usimamizi wa hali za dharura nchini humo kuzuru jimbo la Kentucky na kufanya tathmini ya jinsi hali ilivyo huku akiahidi msaada kamili kutoka serikalini. Kama sehemu ya tamko hilo, misaada ya serikali itatolewa kwa watu walioathirika katika maeneo ya Caldwell, Fulton, Graves, Hopkins, Marshall, Muhlenberg, Taylor, na Warren.
Aina ya msaada utakaotolewa
Msaada huo utajumuisha ruzuku kwa ajili ya makazi ya muda na ukarabati wa nyumba, mikopo ya kufidia hasara ya mali isiyo na bima na mipango mingine ya kuwasaidia watu na wamiliki wa biashara kujikwamua kutokana na athari za janga hilo. Hapo jana, gavana wa Kentucky Andy Beshear alitoa ombi rasmi la tangazo hilo la hali ya dharura baada ya vimbunga hivyo vikali kukumba mji wa Mayfield na kuharibu kiwanda cha mishumaa. Rais Biden alipokea ombi hilo na kuliidhinisha katika saa za jioni .
Huku hayo yakijiri, maafisa wa kukabiliana na hali ya dharura, wanaendelea kutafuta manusura wa janga hilo lililosababisha vifo vya watu wengi katika majimbo kadhaa na kuacha miji ikiwa imeharibika. Wakati huo huo, wakati wa mkutano na wanahabari hapo jana mchana, gavana Beshear alisema kuwa kitu cha kwanza wanachopaswa kufanya ni kuomboleza pamoja kabla ya kuanza kujenga upya pamoja.
Msaada umeanza kutolewa
Tayari mamlaka za kimaeneo zimeanza kutoa msaada kwa wakazi waliopigwa na butwaa wanaopekua vifusi vya nyumba zao na biashara zao kutokana na uharibifu mkubwa. Beshear ameliambia shirika la CNN kwamba zaidi ya watu 80 wamekufa katika jimbo hilo pekee wengi wao wakiwa wafanyakazi katika kiwanda hicho cha mishumaa na kwamba idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kupita 100. Baadaye, gavana huyo alisema kuwa mmiliki wa kiwanda hicho anaamini wafanyakazi zaidi wamepatikana na kuongeza kuwa itakuwa bora iwapo idadi ya waliopoteza maisha itapungua lakini akasisitiza kuwa hawezi kuthibitisha hilo.
Takriban watu sita walikufa katika ghala la kampuni ya Amazon katika mji wa Kusini wa Edwardsville katika jimbo la Illinois ambapo walikuwa wakifanya kazi katika zamu ya usiku wakitayarisha bidhaa zilizoagizwa na wateja kabla ya sikukuu ya Krismasi.