Zoezi hilo lenye lengo la kuhakikisha kuwa mipango na mawasiliano baina ya wadau mbalimbali linaimarishwa na kuwepo kwa ushirika wa kutosha miongoni mwa wadau wote muhimu ikiwemo jamii ni matokeo ya mapendekezo ya wataalamu zaidi ya mia tano kutoka nchi za afrika mashariki walioshiriki katika vita vya ebola katika mataifa kadhaa ya Afrika ,magharibi hivi karibuni.
Wajumbe wa mkutano huo wamesema kumekuwa na mawasilino duni katika mipango ya kukabiliana na dharura za milipuko ya magonjwa kupitia mipakani jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limesababisha madhara makubwa ikiwemo upotevu wa maisha na rasilimali zingine.
Mpango huo shirikishi ukijulikana kwa kimombo ONE HEALTH pamoja na mambo mengine umeshirikisha viongozi wa kijamii ambao wanasema athari za milipuko zimekuwa na madhara kutokana na wananchi kukosa taarifa muhimu kuhusu magonjwa ya milipuko.
Mpango huo mahususi kwa nchi za Afrika Mashariki ambao umetengenezwa chini ya ufadhili wa serikali ya ujerumani kupitia shirika la misaada la taifa hilo GIZ kitengo cha utayari kukabiliana na magonjwa ambukizi utasaidia kuzijengea uwezo idara za dharura za kukabiliana majanga katika nchi wanachama wa mtengamano wa Afrika Mashariki.
Akizungumza katika mkutano huo mkuu wa kituo cha kudhibiti magonjwa katika Umoja wa Afrika Dk. Merawi Aragaw amesifu jitahada za jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kufikia hatua ya kuwa mpango wa pamoja kudhibiti magonjwa katika mipaka na kusema kuwa umoja wa huo umekuwa ukisisitiza kuwepo kwa mazoezi ya nadharia ya kujipima uwezo wa kudhibiti majanga ya magonjwa ya milipuko.
Mpango huo litaangalia namna vyombo vya habari ,viogozi wa dini na kijamii wanavyoweza kushiriki katika mapambano ya magonjwa ambukizi kwa kuweka mipangilio ya kupasha habari na kutoa ujumbe wa tahadahari kwa wananchi mara magonjwa ya milipuko yanapotokea.
Mkutano huo pia umehudhuriwa na wawakilishi wa mashirika ya umoja wa mataifa ya afya na kilimo na chakula pamoja na umoja wa Afrika.
Mwandishi: Charles Ole Ngereza
Mhariri: Mohammed Abdulrahman