1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjuwe Uhuru Kenyatta, mgombea urais wa Jubilee

7 Agosti 2017

Uhuru Muigai Kenyatta ni rais wa sasa wa Kenya na mwanawe Jomo Kenyatta, mwanzilishi na rais wa kwanza wa Jamhuri ya Watu wa Kenya aliyeitawala nchi hiyo ya Afrika Mashariki kuanzia  mwaka 1964 hadi 1978.

https://p.dw.com/p/2fBsv
Uhuru Kenyatta Präsident Kenia Rede Parlament Nairobi
Picha: Getty Images/AFP/S. Maina

Familia yake Uhuru ni ya watu wa  kabila la Kikuyu, kabila linaloonekana kuwa na nguvu na usemi mkubwa nchini humo. Uhuru Kenyatta jina lake limetokana na kipindi cha wakati Kenya ilipokuwa ikitarajia Uhuru wake. Uhuru alizaliwa mjini Nairobi tarehe 26 Oktoba mwaka wa1961.

Alisoma elimu yake ya msingi katika shule ya Loreto Convent na mwaka 1969 akasajiliwa katika shule ya Saint Mary's mjini Nairobi. Kati ya mwaka 1979 na 1980 alifanya kazi katika benki ya Kenya Commercial. Baada ya hapo alielekea Marekani alikosomea uchumi na sayansi ya kisiasa katika shule ya Amherst na baada ya kufuzu 1985 akarejea nchini Kenya.

Kuingia kwake katika siasa ni kupitia kule kuchaguliwa kwake mwaka 1996, kama mwenyekiti wa chama kilichokuwa uongozini wakati huo KANU, ila tawi la mji ambao ni chimbuko lake na ni hatua iliyotiwa kidole na rais wa wakati huo Daniel arap Moi na wengi waliliona jambo hilo kama mwanzo wa mambo makubwa kwa Uhuru katika siasa. 

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1997, Uhuru aliwania kiti cha ubunge wa Gatundu kilichokuwa kikishikiliwa na babake wakati mmoja ingawa alishindwa na mhandisi mmoja wa Nairobi Moses Mwihia. Mwaka 1999, Moi alimteua Uhuru kuwa mwenyekiti wa bodi ya utalii nchini Kenya na mwaka 2001 aliteuliwa kama mbunge na akapewa wadhfa wa waziri wa serikali za mitaa. Mwaka huo huo, alichaguliwa kama mmojawapo wa wenyekiti wanne wa kitaifa wa chama cha KANU.

Kenia Wahlkampf | Uhuru Kenyatta
Picha: Reuters/T. Mukoya

Mwaka 2002, rais mstaafu Moi alitumia ushawishi wake kumteua Uhuru kama mgombea wa urais wa chama cha KANU, jambo lililozusha minong'ono kutoka kwa wanasiasa wengine waliokuwa wanaiwania nafasi hiyo, jambo lililochangia wanasiasa wengi wa KANU kukihama chama hicho.

Hatua ya kumchagua Uhuru ilionekana na wengi kama ya upendeleo na kama mbinu tu ya kumfanya Moi aendelee kuitawala Kenya hata baada ya kustaafu ili aweze kuyaficha yale mabaya aliyoyafanya wakati wa uongozi wake.

Katika uchaguzi huo Uhuru alimaliza wa pili nyuma ya Mwai Kibaki na alikiri kushindwa na akachukua kikamilifu jukumu la kuwa kiongozi wa upinzani. Mwaka 2005, alimshinda Nicholas Biwott katika uchaguzi wa KANU na kuwa mwenyekiti na baada ya hapo akaungana na chama cha Liberal Democratic Party LDP, kilichouasi uongozi wa Kibaki na pamoja wakaipinga rasimu ya katiba iliyokuwa imependekezwa na huko kuangushwa kwa rasimu hiyo ya katiba kiliutia uongozi wa Kibaki aibu kubwa.

Huku uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 ulipokuwa ukikaribia, Uhuru alikiongoza chama cha KANU kubuni muungano na kile cha Party of National Unity chake Mwai Kibaki aliyekuwa anawania muhula wa pili kwa kushindana na Raila Odinga. PNU ilishinda uchaguzi huo uliokumbwa na utata na utata huo ulizusha machafuko yaliyopelekea vifo vya maelfu ya watu kwa kuwa chama cha ODM chake Raila Odinga kilipinga matokeo ya uchaguzi huo.

Kilichofuata ni kubuniwa kwa serikali ya muungano ambapo Kibaki alipewa wadhfa wa rais, naye Raila Odinga akawa Waziri Mkuu na Uhuru Kenyatta akawa chaguo la kwanza la Kibaki kama naibu Waziri Mkuu na akampa wadhfa wa waziri wa fedha katika baraza lake la mawaziri.

Kenia Wahlkampf | Uhuru Kenyatta
Picha: Reuters/T. Mukoya

Kiongozi wa mashtaka katika mahakama ya kimataifa ya ICC, Luis Moreno Ocampo alimfungulia mashtaka Uhuru aliyekuwa kiongozi pia katika chama cha PNU kama aliyehusika japo sio moja kwa moja katika machafuko ya baada ya uchaguzi mwaka 2007 na 2008, na mashtaka hayo yakathibitishwa Januari 23 mwaka 2012.

Ocampo pia alimfungulia mashtaka William Ruto aliyekuwa katika chama cha ODM, kilichokuwa mpinzani mkuu wa PNU katika uchaguzi wa mwaka 2007. Uhuru aliachia ngazi kutoka wadhfa wake wa waziri wa fedha kufuatia kuthibitishwa kwa mashtaka hayo ingawa alisisitiza kwamba hana hatia. Mashtaka hayo dhidi ya Uhuru yaliondolewa tarehe 13 Machi mwaka 2015 kwa ukosefu wa ushahidi.

Tarehe 20 Mei mwaka 2012, Uhuru alihudhuria uzinduzi wa chama cha The National Alliance TNA na uwepo wake katika uzinduzi huo uliwapelekea wengi kuhisi kwamba atawania uteuzi wa chama hicho kwa kuuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2013 nchini Kenya.

Waziri wa haki na masuala ya sheria nchini Kenya wakati huo Eugene Wamalwa pamoja na mbunge wa Eldoret Kaskazini wakati huo William Ruto waliongoza zaidi ya wabunge 70 kuhudhuria uzinduzi huo.

Chama cha TNA chake Uhuru Kenyatta kiliungana na kile cha United Republican Party URP, Republican Congress Party chake Najib Balala na National Rainbow Coalition NARC chake Chairty Ngilu na wakabuni muungano wa Jubilee Alliance.

Kenia Nairobi Präsident Kenyatta und Team Leichtathletik für Rio
Picha: Reuters/T. Mukoya

Uchaguzi ulipofanyika Uhuru alitangazwa kuwa rais tarehe 9 Machi ambapo alimbwaga Raila Odinga aliyeuongoza muungano wa Coalition for Reform and Democracy CORD.

Matokeo ya uchaguzi huo yalipingwa na muungano wa CORD ingawa kesi waliyoiwasilisha mbele ya mahakama ya juu zaidi nchini Kenya, ilimpa ushindi Uhuru Kenyatta. 

Katika uongozi wake Uhuru Kenyatta amekuwa na mafanikio kiasi cha haja ingawa changamoto nazo hazijakosekana na ameshutumiwa mara kadhaa kuchangia katika masuala ya kikabila. 

Mwaka 2015 gazeti moja kuu nchini Kenya lilisema kwamba yeye ndiye rais aliyesafiri nje ya nchi mara nyingi zaidi akilinganishwa na watangulizi wake ambapo kufikia Novemba 2015, alidaiwa kusafiri mara 43 katika kipindi cha miaka mitatu, ambapo Mwai Kibaki alisafiri mara 33 tu nje ya nchi katika kipindi cha miaka 10.

Atawania urais kwa muhula wa pili na iwapo atashinda basi utakuwa ni muhula wake wa mwisho kwani katiba ya Kenya inamtaka rais kuongoza kwa kipindi cha mihula miwili tu. Mgombea wake mwenza atakuwa ni William Ruto ambaye ni makamu wake kwa sasa.

Mwandishi: Jacob Safari
Mhariri: Iddi Ssessanga