Mjumbe wa UN aliyeamriwa kuondoka Somalia aonya kuhusu fujo
4 Januari 2019Mjumbe wa Umoja wa Mataifa aliyeamriwa kuondoka hivi karibuni nchini Somalia ameonya dhidi ya machafuko ya kisiasa kwenye taifa hilo la Pembe ya Afrika, huku balozi wa Somalia kwenye Umoja huo akilitaka Baraza la Usalama kuacha kuingilia mambo ya ndani ya nchi yake.
Wakizungumza kwenye kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo jana, wawili hao walitoa kauli zinazohitafiliana, siku mbili baada ya Somalia kumuamuru Nicholas Haysom kuondoka nchini humo, ikimtuhumu kwa kukiuka mipaka ya kazi yake.
Haysom aliliambia Baraza la Usalama kwamba hali ya kisiasa nchini Somalia inatishia kulitumbukiza tena taifa hilo kwenye machafuko makubwa.
Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa alifukuzwa baada ya kuhoji kukamatwa kwa watu kadhaa, akiwemo Mukhtar Robow, kiongozi wa zamani wa kundi la kigaidi la al-Shabaab.
Balozi wa Somalia kwenye Umoja wa Mataifa aliliambia Baraza la Usalama kwamba licha ya nchi yake kushukuru kwa msaada wa Umoja huo, lakini ina haki ya kuheshimiwa masuala yake ya ndani.