Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen ajiuzulu
16 Aprili 2015Hii ni baada ya miaka minne ya juhudi za kufanikisha kipindi cha mpito wa kisiasa kwa njia ya amani katika taifa hilo maskini zaidi la ulimwengu wa Kiarabu kusambaratika, wakati kukiwa na uasi unaofanywa na wapiganaji wa Kishia na mashambulizi ya anga yanayoongozwa na Saudi Arabia.
Taarifa ya Umoja wa Mataifa imesema Jamal Benomar ameelezea nia yake ya kujiuzulu na kuchukua jukumu jingine na mrithi wake atatangazwa katika siku chache zijazo. Benomar alijikuta chini ya shutuma kali kutoka baadhi ya mataifa ya Mashariki ya Kati na hasa Saudi Arabia, wakati juhudi zake za kutafuta amani kutopata mafanikio makubwa. Mara kwa mara alikuwa akiwasilisha taarifa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali nchini Yemen na pia alitambulika sana na wanadiplomasia wengi.
Haijafahamika wazi kama mwanadiplomasia wa Mauritania Ismail Ould Cheikh Ahmed huenda akachukua nafasi ya Benomar. Duru ya kidiplomasia ya Umoja wa Mataifa imesema uteuzi wake haujathibitishwa bado na huenda ukabadilishwa. Mwezi Januari mwaka jana, Ould Cheikh Ahmed aliteuliwa kuwa naibu wa mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Libya na kisha mwezi Desemba akapewa jukumu la kuongoza ujumbe wa Umoja wa Mataifa kushughulikia mlipuko wa ugonjwa wa Ebola UNMEER.
Wakati huo huo, Saudi Arabia na Misri zinatafakari kuandaa mazoezi makubwa ya kijeshi baada ya kufanya mashambulizi ya kutokea angani dhidi ya waasi wa Yemen ambao Umoja wa Mataifa umewawekea vikwazo na kupiga marufuku wao kupewa silaha.Msemaji wa jeshi la Saudi Arabia Brigadier Jenerali Ahmed Asiri amesema manowari za jeshi la muungano zinaendelea na operesheni ya kuzikagua meli zinazosafiri katika mwambao wa Yemen ili kuzuia silaha kuwafikia wasi.
Yemen inaendelea kukumbwa na mashambulizi ya anga yanayoongozwa na Saudi Arabia katika jaribio la kuwasogeza nyuma waasi wa Kishia wa Houthi ambao wameyakamata maeneo mengi ya kusini kutokea eneo lao karibu na mpaka wa Saudia na kumfanya rais wa Yemen kukimbilia mjini Riyadh. Zaidi ya watu 700 wameuawa tangu mashambulizi hayo yalipoanza.
Baraza la Ushirikiano wan chi za Ghuba – linalowajumuisha majirani wa Yemen Saudi Arabia na Oman pamoja na Bahrain, Kuwait, Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu – liliunda mpango wa kuwepo kipindi cha mpito wa kisiasa nchini Yemen ambao ulitekelezwa kwa sehemu tu.
Saudi Arabia inaishtumu Iran – ni dola lenye nguvu la washia – kwa kuwapa silaha waaasi na mzozo huo wa Yemen umeongeza mivutano katika Mashariki ya Kati. Rais wa Iran Hasan Rouhani anasisitiza kuwa Iran haitaki kuitawala kanda hiyo.
Mwandishi wa habari: Bruce Amani/AP
Mhariri:Yusuf Saumu