1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa kuikwamua Burundi katika mgogoro

22 Novemba 2018

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Burundi ameshauri kutathminiwa upya kwa njia za kuisaidia Burundi kujikwamua kwenye mgogoro wa kisiasa, kwa mtizamo wa uchaguzi unaotarajiwa mwaka 2020

https://p.dw.com/p/38hkk
Michel Kafando
Picha: UN/Manuel Elias

Mjumbe huyo Michel Kafando ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba tofauti bado zinashuhudiwa kati ya serikali na upinzani, na kwamba hakuna uaminifu kati yao, na matamshi ya chuki dhidi ya wapinzani yanaendelea kutolewa. Burundi ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa kufuatia tangazo la Rais Pierre Nkurunziza mwezi Aprili mwaka 2015, kwamba atawania urais kwa muhula wa tatu.

Kura ya maoni ya mwaka huu iliidhinisha mabadiliko ya katiba ambayo yatamruhusu Rais Nkurunziza ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2005, miaka kumi na nne baada ya muhula wake wa sasa kukamilika mwaka 2020. Lakini mwezi Juni mwaka huu, alitangaza kuwa hatowania tena urais na atamuunga mkono atakayeshinda uchaguzi ujao.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterress amesema katika ripoti mpya kwa Baraza la Usalama la umoja huo kwamba tangu mwezi Agosti, hali ya usalama imesalia kuwa ya utulivu, licha ya polisi kukamata bunduki na risasi, pamoja na kuripotiwa kwa visa vya mauaji , kukamatwa kiholela na kutoweka kwa raia. Vile vile ametaja ripoti za mashambulizi katika vijiji na misismamo ya majeshi na watu wasiojulikana na ambao walijihami kwa silaha.

Antonio Guterres
Picha: picture-alliance/Photoshot/Li Muzi

Guterres amesema uamuzi wa serikali wa kutohudhuria mkutano wa tano wa mazungumzo kuhusu Burundi tarehe 25 mwezi Oktoba mwaka huu, na mazungumzo yenyewe kukosa kupiga hatua katika upatikanaji wa azimio la kudumu kwa mgogoro wa mwaka 2015, linasalia kuwa suala linalotia wasiwasi mkubwa.

Amesisitiza kwamba huku mazungumzo y kisiasa yakibadilika na kuangazia zaidi matayarisho ya uchaguzi wa mwaka 2020, pande zote zinafaa kujua kuwa amani ya kudumu inaweza tu kupatikana na kudumishwa iwapo moyo wa maelewano na kanuni za sheria zitazingatiwa katika uongozi wa nchi.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Burundi Michel Kafando amesema licha ya baadhi ya vyama kuiunga mkono serikali bado nafasi ya demokrasia imeendelea kuwa kikwazo nchini Burundi. Kafando amesema hali bado ni tete sio tu kutokana na ukosefu wa mazungumzo ya kisiasa ya pamoja lakini kwasababu ya matatizo ya kibinadamu, uchumi na fedha, vile vile vitisho vya kiusalama.

Burundi Botschafter Albert Shingiro in Bujumbura
Picha: Getty Images/AFP/G. Tapper

Baada ya miaka mitatu ya juhudi za kufanikisha mazungumzo, Kafando amesema Waburundi wenyewe wanafaa kutathmini upya njia za kusitisha mgogoro wa kisiasa. Wakati uo huo amesema jamii ya eneo la Afrika Mashariki inafaa kufanya tathmini wakati wa mkutano wao mkuu.

Kwa upande wake Balozi wa Umoja wa Mataifa nchini Burundi Albert Shingiro ameitaja hali nchini humo kuwa tulivu, imara, na iliyodhibitiwa akisema mgogoro wa mwaka 2015 umesahaulika. Aidha ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa uchaguzi wa mwaka 2020 utafadhiliwa na raia wa Burundi na utakuwa wa kidemokrasia na kusisitiza kwamba matayarisho ya uhaguzi wenyewe yanafanyika katika hali tulivu na shwari.

Mwandishi: Sophia Chinyezi/APE

Mhariri: Saumu Yusuf