Mjumbe wa Umoja wa Mataifa afanya mazungumzo Tripoli
2 Januari 2016Martin Kobler, ambaye anafanya juhudi za kidiplomasia kuzishawishi serikali mbili pinzani za Libya kusaini mpango wa kugawana madaraka, alikutana siku ya Alhamisi na wawakilishi wa serikali inayotambuliwa na jamii ya kimataifa karibu na makao yake makuu mashariki mwa nchi hiyo. Kisha jana akakutana na Nouri Abusahmein, mkuu wa bunge pinzani la Tripoli. Libya imekuwa katika machafuko tangu kuondolewa madarakani mwaka wa 2011 aliyekuwa kiongozi wa muda mrefu Muammar Gaddafi na sas ina serikali mbili na mabunge mawili.
Makundi ya jihadi kama vile Dola la Kiislamu yamechukua nafasi hiyo ya kukosekana utawala thabiti kuingia katika ukanda wa pwani, na Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa mapigano yamewalazimu watu 435,000 kukimbia makazi yao.
Mnamo Desemba 17 mwaka jana, chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa, wajumbe kutoka pande zote na viongozi kadhaa wa kibinafsi walisaini mpango wa kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa.
Karibu wabunge 80 kati ya 188 kutoka bunge la Libya linalotambuliwa kimataifa na 50 kati ya 136 wa bunge pinzani lenye makao yake mjini Tripoli walisaini muafaka huo. Unatoa wito wa kuundwa serikali ya mawaziri 17, inayoongozwa na mfanyabiashara Fayez el-Sarraj kama waziri mkuu, na kuwa na makao yake mjini Tripoli.
Lakini wachambuzi wanaelezea shaka kuhusu utekelezwaji wa muafaka huo ambao utahitaji kuyaleta pamoja mabunge mawili yanayodhibitiwa na watu wenye misimamo mikali.
Abusahmein amemwomba Kobler kukutana na viongozi kadhaa wa serikali ya Tripoli, wakiwemo maafisa wakuu wa jeshi na ujasusi na mahakama. Kobler amesema walikubaliana kuhusu mambo matano kwenye mkutano wake na Abusahmein hapo jana .
Kwanza makubaliano ya kisiasa kuhusu Libya yanahitaji majadliano ya pande zote. Hakuna mbadala wa hilo. Pili, hakupaswi kuwa na mipango sambamba. Mipango yote inapaswa kuwa chini ya mwmvuli wa Umoja wa Mataifa.
Mchakato huo lazima uzijumuishe pande zote na pia kuongozwa na kanuni ya “kukabidhiwa kwa njia ya amani madaraka kutoka kwa taasisi za zamani hadi kwa taasisi mpya”.
Na kisha Kobler akamalizia kwa kusema kuwa kuna kanuni ya umili wa Libya. Maana kuwa mpango huo unapaswa kuwa wa Walibya na Walibya wenyewe lazima wauongoze mchakato huo.
Hata hivyo kikao hicho cha waandishi habari cha Kobler katika uwanja wa ndege mjini Tripoli kilikatizwa ghafla na Jamal Zoubia, mkuu wa idara ya habari katika serikali yenye makao yake mjini Tripoli, aliyemwambia Kobler kuwa kikao hicho hakikuwa halali kwa sababu alihitaji idhini kwanza.
Mwandishi: Bruce Amani/AFPE
Mhariri: Sekione Kitojo