1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjumbe wa Marekani kuzuru Saudi Arabia, Sudan na Ethiopia

Zainab Aziz Mhariri: Tatu Karema
15 Januari 2022

Mjumbe maalum wa Marekani anayeshughulikia maswala ya Pembe ya Afrika atafanya ziara kwenye mataifa matatu wiki ijayo. Nchi hizo ni Saudi Arabia, Sudan na Ethiopia.

https://p.dw.com/p/45a4i
Saudi-Arabien Riyadh | Palast | Gulf Cooperation Council
Picha: Bandar Aljaloud/Saudi Royal Palace/AP/picture alliance

Mjumbe huyo David Satterfield ataandamana naibu waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Molly Phee na ziara yao inajiri huku kukiwa na migogoro inayoendelea katika mataifa mawili ya Kiafrika ya Ethiopia na Sudan.

Wizara ya Mambo ya Nje ya marekani imesema ziara ya mjumbe David Satterfield na Phee itaanza tarehe 17 hadi tarehe 20 Januari ambapo wataanzia mjini Riyadh, Saudi Arabia ambako watakutana na "Friends of Sudan”, kundi linalotaka kurejeshwa kwa serikali ya mpito nchini humo tangu yalipofanyika mapinduzi ya kijeshi mnamo mwezi Oktoba mwaka uliopita.

Mwana Mfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman Al Saud
Mwana Mfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman Al SaudPicha: BARNI Cristiano/ATP photo agency/picture alliance

Mkutano huo unalenga kutafuta kuungwa mkono kimataifa kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya  kuwezesha mabadiliko mapya nchini Sudan chini ya uongozi wa kiraia unaotarajiwa kufanikisha nchi hiyo kurejea kwenye demokrasia.

Baada ya hapo Satterfield na Phee wataelekea mji mkuu wa Sudan, Khartoum, ambapo watakutana na wanaharakati wanaounga mkono demokrasia, makundi ya wanawake na vijana, mashirika ya kiraia, wanajeshi na viongozi wa kisiasa.

Na huko watatoa ujumbe wao wa wazi kwamba Marekani inasisitiza na inaunga mkono uhuru, amani na haki kwa watu wa Sudan.

Na kumalizia ziara yao watakwenda nchini Ethiopia, ambako watafanya mazungumzo na Waziri Mkuu Abiy Ahmed kutafuta suluhisho la hali mbaya inayosababishwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya marekani imesema mjumbe huyo maalum anayeshughulikia maswala ya Pembe ya Afrika David Satterfield na naibu waziri wa Wizara ya Mambo Nje Molly Phee   watawahimiza maafisa wa serikali kuchukua fursa iliyopo sasa kuleta amani nchini Ethiopia kwa kusimamisha mashambulio ya anga na uhasama mwingine.

Kuanzishwa hatua za kusitisha mapigano

Pia watapendekeza kuanzishwa hatua za kusitisha mapigano, kuachiwa kwa wafungwa wa kisiasa na kurejeshwa shughuli za kupeleka misaada.

David Satterfield, ambaye zamani alikuwa balozi wa Marekani nchini Uturuki, aliteuliwa kuchukua nafasi ya Jeffrey Feltman mnamo Januari 6.

Feltman alijiuzulu mara tu alipoitembelea Ethiopia kwa ajili ya kuhimiza mazungumzo ya amani kumaliza vita vya zaidi ya mwaka mmoja baada ya kundi la TPLF lilipowasimamisha wapiganaji wake kuendelea na mapigano.

Kundi hilo la Ukombozi wa Watu wa Tigray TPLF, mwaka jana lilitishia kuingia kwenye mji mkuu wa Addis Ababa kufikia Desemba lakini liliamua kuondoka na kurudi kwenye ngome yake katikam jimbo lenye lenye mzozo la Tigray.

 Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed Ali
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed AliPicha: Minasse Wondimu Hailu/AA/picture alliance

Jeffrey Feltman pia alijaribu kuutatua mzozo wa Sudan, lakini alihisi kutotendewa vyema mnamo mwezi Oktoba wakati mtawala wa kijeshi wa Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, alipofanya mapinduzi mara tu baada ya mjumbe huyo wa Marekani kuondoka nchini humo.

 Alijiuzulu siku chache baada ya waziri mkuu wa kiraia wa Sudan, Abdalla Hamdok, kujiuzulu, na kumwacha Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, kama kiongozi wa Sudan asiye na mpinzani licha ya wito wa nchi za Magharibi wa kutaka makubaliano ya kipindi cha mpito ya kidemokrasia yaliyoanzishwa mwaka 2019 yaendelee kufanya kazi.

Chanzo:AFP